Keshokutwa Oktoba 14, 2016 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anatimiza miaka 17 tangu afariki dunia Oktoba 14, 1999 katika hospitali ya Mtakatifu Thomas, London, Uingereza  alikokuwa amelazwa akitibiwa ugonjwa wa saratani ya damu.

Wakati wa uhai wake Baba wa Taifa alifanya kazi nyingi na kubwa ndani na nje ya nchi ili kupigania ukombozi, umoja, mshikamano pamoja na kuwaelimisha Waafrika kuhusu haki zao. Katika harakati hizo, hasa za ukombozi wa Afrika, mwanzoni mwa 1971 aliamua kuanzisha Jeshi la Anga ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Aliwapeleka vijana wa Kitanzania nchini China kufanya mafunzo ya utaalamu wa ndege za kivita wakiwamo marubani na wahandisi wa fani zote muhimu kama radar, mawasiliano na hali ya hewa. Hicho kilikuwa kipindi ambacho Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa alikuwa Edward Moringe Sokoine na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) alikuwa Meja Jenerali Mirisho Sarakikya, Kamanda wa kwanza wa kikosi hicho cha anga akiwa Luteni Kanali James Luhanga.

Ni Luhanga aliyesimamia mafunzo yote ya Jeshi la Anga tokea Januari 1971 hadi Septemba 1973 wataalamu hao walipomaliza mafunzo yao ya kurusha na kutengeneza ndege za kivita. Hatua hiyo ilikuwa historia kubwa katika JWTZ tokea jeshi hilo lianzishwe rasmi mwaka 1964. Tangu mwaka 1964, JWTZ halikuwa na Jeshi la Anga wala Jeshi la Wanamaji (Airforce na Navy) mpaka 1973 ndipo JWTZ lilipoanza kukamilisha kwa kuwa na majeshi muhimu kama wapiganaji wa ardhini (infantry), wanaanga na wanamaji.

Dar24.com imezungumza na mmoja wa wanafunzi waanzilishi wa Jeshi la Anga, mhandisi msataafu Japhet Mwandimo, ambaye amesema kwamba japokuwa wanajeshi wa kwenye ardhi walikuwa na mizinga, lakini mizinga hiyo haikuwa inaweza kushambulia na kutungua ndege za kivita zenye mwendo kasi.

Anasema wakati huo hakukuwa na mizinga ya kutungulia ndege za kivita kwa kutumia makombora hivyo JWTZ walikuwa wanapata shida sana kukabiliana na ndege za kivita za Wareno waliokuwa wakipambana na wapigania Uhuru wa Msumbiji wakiongozwa na Samora Machel chini ya chama cha kupigania Uhuru cha Frelimo.

Kwa mujibu wa Mwandimo baadhi ya makamanda wa Frelimo walipokuwa wakiona mashambulizi ya ndege za Wareno yanakuwa makali walikuwa wanakimbilia Tanzania katika Mkoa wa Mtwara maeneo ya Kitaya na Newala.

Huko kulikuwa na mizinga ya JWTZ iliyotumika kutungua ndege hizo ili kupunguza kasi ya Wareno katika kufanya mashambulizi hasa katika maeneo ya Wilaya ya Nachingwea. Anasema vijana wataalamu wa ndege za kivita waliotoka mafunzoni China hadi Oktoba 1973 walikuwa wamefanya mafunzo ya kutosha: kuruka mchana na usiku; kupambana angani, ardhini na baharini.

Desemba 9, 1974 Bara ilitimiza miaka 13 tangu ipate Uhuru kutoka kwa ukoloni wa Waingereza. Lakini pia ilitimiza miaka 10 ya kuundwa kwa JWTZ. Sherehe hizo ziliunganishwa na walialikwa wageni wengi, akiwamo Sarakikya na Gavana wa mwisho wa Tanganyika ya mkoloni, Sir Richard Turnbull. Wageni wengine waliohudhuriwa ukiacha wa ndani ni pamoja na wapigania uhuru kutoka vyama vya ukombozi vya ANC, Afrika Kusini; Frelimo, Msumbiji; MPLA, Angola; Zanu PF, Zimbabwe; Swapo, Namibia na vinginevyo vilivyokuwa na wawakilishi nchini. Kwa mara ya kwanza katika sherehe hizo zilizofanyika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru), JWTZ ilirusha ndege za kivita aina ya F6 (Fighter Six) ambazo zilikuwa na kasi kubwa na uwezo wa kubeba mabomu zaidi ya tani moja na makombora ya kutungulia ndege za adui pamoja na mizinga mitatu ya mashambulizi.

Kwa miaka hiyo, ndege hizo katika Bara la Afrika zilikuwa adimu. Ni majeshi ya Misri, Sudan, Zambia na Libya pekee yaliyokuwa na ndege za aina hiyo. Uwezo wake ulikuwa unafanana na Phantom Four (F4) za Kimarekani au Mig 19 za Kirusi. Vijana wa Kitanzania na JWTZ walirusha ndege zipatazo 14 kwa wakati mmoja kwenye sherehe hizo. Lilikuwa ni onyesho kubwa lililotangaza uwezo wa jeshi la anga la Tanzania.

Haikuwa ajabu kwamba mwaka 1975 Wareno walitoa Uhuru kwa Msumbiji na Angola. JWTZ lilikuwa limeharakisha kupatikana kwa uhuru katika nchi hizo za kusini mwa Afrika. Jeshi la Anga lilichangia sana katika Vita ya Kagera na pia katika kuwazuia Makaburu wasishambulie vituo vya wapigania uhuru wa ANC/SWAPO/ZANUPF waliokuwa Tanzania katika Mikoa ya Ukanda wa Kusini mwa Tanzania. JWTZ lilikuwa tayari kwa ajili ya mashambulizi ya ndege hizo ambazo ni sawa za walizotumia Marekani kushambulia Libya kwenye miji ya Benghazi na Tripoli wakitokea kwenye visiwa vya Sicilly na Malta wakati wa utawala wa Ronald Reagan.

Akizungumzia vita ya Kagera Mwandimo amesema jeshi la Tanzania la anga lilitoa mchango mkubwa sana kwa kulinda anga  katika Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Shinyanga na Arusha kwani ndege za kivita za Uganda aina ya Mig 21 na Tupolev ambazo walipewa na Gadaffi zilikuwa na uwezo wa kuishambulia mikoa hiyo na kurudi Entebbe kutokana na uwezo wa ndege hizo, lakini walishindwa kufanya hivyo kwa kuwa Tanzania ilikuwa tayari wakati wote wa vita kwa maana wao wakirusha ndege Entebbe na Tanzania ilikuwa inarusha ndege kuelekea kwenye mipaka yake ya Uganda na hasa katika mikoa ya Kagera na Musoma ambayo imepakana na Uganda pamoja na Ziwa Victoria.

Idd Amin kwa kiasi kikubwa alisaidiwa sana na Muamar Gadaffi hivyo kuna ndege zingine zilikuwa zinatoka Libya moja kwa moja kuja kuishambulia Tanzania lakini Jeshi la Anga katika kufuatilia mienendo yao chini ya Jenerali Robert Mboma lilikuwa imara na kuwashinda. Wakati vita inakaribia kwisha yalifanyika mashambulizi makali katika miji ya Entebbe, Jinja na Kampala ili kuwakatisha tamaa askari wa Amin na Gadaffi ambao ndio walikuwa katika mapambano hadi mwisho wa vita Aprili 1979.

Majeshi na raia wa Tanzania walikuwa wamehamasika sana na kauli za Amri Jeshi Mkuu, Mwalimu Nyerere ambazo zitachukua muda mrefu kusahaulika miongoni mwa wapiganaji. Kauli hizo ni pamoja na: UWEZO TUNAO, SABABU TUNAYO NA NIA TUNAYO ya kumpiga nduli IDD AMIN na majeshi yake. Katikati ya vita Gadaffi alitangaza kumsaidia Amin na kumtaka Mwalimu Nyerere ayaondoe majeshi yake nchini Uganda katika muda wa saa 48 la sivyo Libya ingeingia vitani kwa upande wa Uganda.

Mwalimu alimjibu Gaddaffi kuwa asingeweza kuyaondoa majeshi yake Uganda kwa amri ya Gadaffi na badala yake akasema zile zilikuwa ni mvua za rasharasha, za masika zilikuwa mbioni kuanza.

Baada ya vita Gadaffi alimuomba Mwalimu Nyerere amrudishie mateka wake zaidi ya askari 460 kwa gharama yoyote na kwamba Libya ilikuwa tayari kulipa ili askari wake warudi.

Mwalimu Nyerere alimjibu Gadaffi kuwa alikuwa amewasamehe askari wake kwa kuwa walikuwa hawajui watendalo hivyo aje awachukue bure kwa kuwa thamani ya roho ya mwanadamu anaeijua ni Mwenyezi Mungu pekee.

Gadaffi hakuamini maneno hayo mpaka alipotuma ndege zake aina ya Boeing 707 kuja Tanzania na kuwachukua mateka wake wakiwa salama.

Manji Kuwatega Kivingine Wanachama Wa Young Africans
Sergio Aguero Ashindwa Kutimiza Ahadi