Naibu waziri wa madini Stanslaus Nyongo amekanusha uwepo wa vitendo vya udhalilishaji katika mgodi wa madini ya Tanzanite uliopo mererani mkoani Manyara.

Nyongo ametoa kauli hiyo jana katika jukwaa la tisa la asasi za kiraia la mijadala inayoendelea kwenye wiki ya AZAKI jijini Dodoma baada ya mchimbaji mdogo wa madini hayo kutoka jijini Arusha Kanaeli Minja kutoa malalamiko.

Mchimbaji huyo ameeleza kuwa licha ya Serikali kutoa mwongozo wa kufungwa kwa mashine za ukaguzi hadi sasa bado hazijafungwa na wameendelea kudhalilika kwa kuachwa utupu hata kama wakionesha ushirikiano katika zoezi la ukaguzi ili kuingia mgodini.

“wanawake wanavuliwa nguo na kuachwa utupu mbele ya watoto wadogo hata wakionesha ushirikiano katika zoezi la ukaguzi hali hii si sawa na inapaswa kupigwa marufuku,” amesema Kanaeli.

Kufuatia maelezo yake ameiomba serikali kukemea tabia hiyo na kuwataka viongozi wanaosimamia mgodi huo kufunga mashine hizo kama ilivyoagizwa na serikali ambazo zitarahisisha ukaguzi na kudhibiti utoroshwaji wa madini na kuondoa udhalilishaji.

Akitoa ufafanuzi wa malalamiko hayo Naibu Waziri Nyongo amesema madai ya Kanaeli hayana ukweli isipokuwa wengi wao wamekuwa hawataki kutoa ushirikiano wakati wa ukaguzi.

“Kuna scanner zinazotumika kukagua madini ni maalum na ni za gharama kubwa zina teknolojia kubwa tumeshaagiza na si kweli kwamba watu wananyanyaswa ila baadhi yao hawataki kutoa ushirikiano wakati wa ukaguzi,” amebainisha Nyongo.

Wiki hiyo ya asasi za kiraia (AZAKI) ilizinduliwa Novemba 4, 2019 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na itahitimishwa rasmi Novemba 8, 2019 hapa jijini Dodoma.

LIVE: Rais Magufuli akifungua Mkutano wa Mawaziri Afrika na Nordic
Video: Steve Nyerere amvaa Zahera: Anachofanya ni utoto/mambo yake ya ndani/tumefiwa

Comments

comments