Nyota ya kocha wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer imeendelea kuwaka akiwapa ushindi mfululizo wekundu hao wa Old Trafford unaokausha vidonda vya vipigo walivyokuwa wakivipokea.

Jana, Manchester United ikiongozwa na Solskjaer ilifanikiwa kugawa kipigo cha 2-0 dhidi ya Newcastle United na kuandika historia ya aina yake.

Kutokana na ushindi huo wa jana, Solskjaer amekuwa kocha wa kwanza wa klabu hiyo tangu miaka 72 iliyopita, kufanikiwa kushinda michezo yake ya kwanza minne mfululizo kwenye mechi za Ligi Kuu ya Uingereza.

Kocha huyo ambaye ana historia ya kufanya maajabu akiichezea klabu hiyo miaka kadhaa iliyopita, ameifuata rekodi ya kocha pekee wa Manchester, Sir Matt Busby ambaye aliweka rekodi hiyo mwaka 1946.

Magoli ya Manchester United jana yalifungwa na Romelu Lukaku katika dakika ya 64 akitokea benchi pamoja na Rashford aliyefunga jalada la hukumu ya siku katika dakika ya 80.

Ushindi huo umeisogeza Klabu hiyo ingawa bado inabaki katika nafasi ya sita ya msimamo wa Ligi ikiwa na alama 38.

“Unaweza kuwa na furaha sasa kwa ushindi mara nne mfululizo. Tulianza taratibu katika kipindi cha kwanza lakini tulimiliki mchezo. Tulikuwa makini na kwa ujumla tulicheza kitaalam sana,” alisema Solskjaer.

 

Kocha wa Newcastle United, Rafael Benitez ameeleza kuwa wamepokea kichapo hicho kutokana na makosa waliyoyafanya wakicheza dhidi ya timu yenye wachezaji wazuri.

“Tulikuwa na nafasi kadhaa laini tulifanya makosa na walituadhibu, hii hutokea pale unapocheza na timu yenye wachezaji wazuri,” alisema. Benitez.

Newcastle ina hali ngumu ikiwa na alama 18 inayoiweka kwenye nafasi ya 15 ya msimamo wa Ligi.

Waziri Mkuu atoa agizo kwa viongozi Ruvuma, ni kuhusu elimu
Zuma azua mvutano baada ya kupewa msaada wa kurekodi albam yake