Ajuza mmoja mkazi wa kijiji cha Mgungia Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Fatuma Mussa maarufu kwa jina la Nyamgoma (78), amefariki baada ya kuumwa na nyuki akidaiwa kukaidi amri ya kukatazwa kutoka nje ya nyumba.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho ambaye pia ni shuhuda wa tukio la kuumwa na nyuki kikongwe huyo, Said Mayunga ameeleza kuwa walikwenda kwenye mji wa Hassani Ramadhani kwa mwaliko wa kumsaidia kujenga makaburi na baada ya kazi hiyo walifanya Dua ya kuwaombea marehemu, hivyo nyuki waliokuwa wameweka makazi kwenye nyumba hiyo walianza kutoka  baada ya kuona moshi uliotokana na kuni walizokuwa wanapikia.

Baada ya nyuki hao kuanza kutoka  watu wote waliokuwepo kwenye nyumba hiyo  walitahadharishwa na mwenye mji kufanya  shughuli zao kwa tahadhari kukwepa madhara ya nyuki hao. Imeelezwa kuwa ilipofika majira ya saa 9:30 mchana nyuki hao walikuwa tayari wametanda sehemu hiyo tayari kwa mashambulizi, na kuanza kumshambulia mtu mmoja mmoja aliyekuwa nje ya nyumba hiyo, ajuza Fatuma aliyekuwa ndani alipokuwa akitoka alionywa asiondoke lakini alikataa akajifunga vizuri nguo zake, akatoka nje ili aende kwake.

“Lakini ghafla akazingirwa na kundi kubwa la nyuki, akaanza kuumwa, akaanguka chini, akaanza kupiga kelele kuomba msaada wakati huo nyuki wakiingia mdomoni na masikioni,” alieleza Shuhuda Saidi alipo zungumza na Majira.

Naye mwenyekiti wa kitongoji cha Mgungia, Mbandani Msule amesema kuwa jitihada za kumuokoa zilifanyika kwa wananchi waliokuwa karibu kumfunika na turubai huku wao pia wakiumwa na nyuki hao. Wananchi hao waliendelea kufukiza moshi hadi walipotulia wakampeleka Bibi Fatuma zahanati ya Kaselya alikopewa matibabu na kurudishwa nyumbani.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mgungia, Ismail Gone ameeleza kuwa ajuza huyo alifariki Dunia baada ya kurudishwa nyumbani kwake kutokana na majeraha aliyo yapata.

Beppe Marotta akaribia Inter Milan
Kim Kardashian afunguka kuhusu video yake ya ngono

Comments

comments