Bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula zimetajwa kuchangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwezi unaoishia Novemba 2019 kwa asilimia 3.8

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ruth Minja, alipokuwa akitoa taarifa ya mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Novemba 2019.

Bidhaa hizo ni mchele, nyama, unga wa muhogo, mihogo, mafuta ya kupikia, mboga, maharage, mavazi, mkaa, samani, mazulia na huduma ya malazi ya nyumba za wageni.

“Mahitaji ndiyo yamesababisha kupanda kwa bei za bidhaa hizi na inawezekana inachangiwa na uhaba wa uzalishaji na usafirishaji,” amesema Minja.

Ameeleza baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoongezeka bei kwa Novemba 2019 zikilinganishwa na mwezi Novemba 2018, ni pamoja na mchele kwa asilimia 6.6, unga wa muhogo kwa asilimia 7.8, nyama kwa asilimia 2.6, mafuta ya kupikia kwa asilimia 7.2.

“Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Novemba 2019, imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwapo kwa mwaka ulioishia Oktoba 2019,” amesema Minja.

Katika hatua nyingine amesema kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei ni pamoja na mavazi kwa asilimia 2.7, mkaa kwa asilimia 4.4, samani kwa asilimia 3.1, huduma ya malazi kwenye nyumba za wageni kwa asilimia 5 na mazulia kwa asilimia 6.3.

Aidha amesema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Novemba 2019, umeongezeka hadi asilimia 6.1 kutoka asilimia 5.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba 2019.

Kuhusu mfumuko wa bei  kwa nchi nyingine, Mkurugenzi huyo amesema nchini Kenya mfumuko umeongezeka hadi asilimia 5.56 kutoka asilimia 4.95 kwa mwaka ulioishia Oktoba 2019.

Kenya: Gavana Sonko aachiwa kwa dhamana na masharti magumu
Mfungwa afariki baada ya kupewa msamaha wa Rais

Comments

comments