Serikali wilayani Kilolo imetangaza njia mbadala ya kudhibiti magonjwa ya milipuko kwa kukemea vikali na kuwawekea alama wakazi wanaoishi bila kuwa na choo bora wilayani hapo.

Ambapo katibu tawala wa wilaya ya Kilolo, Yusuph Msawanga amebainisha kuwa wananchi ambao watabainika kutokuwa na vyoo bora watawekewa alama ya bendera nyekundu majumbani kwao kama kiashirio kuonesha nyumba hizo kutokuwa na mfumo bora wa kuhifadhi taka mwili.

Serikali imefikia uamuzi huo ikiwa ni mbinu mojawapo ya kuhamasisha wakazi kumiliki vyoo bora ili kusaidia kutokomeza magonjwa ya milipuko kama homa za matumbo pamoja na kipindipindu.

Hata hivyo katibu tawala amewataka wananchi wilayani hapo kuhakikisha wanajenga vyoo bora kabla ya kufikiwa na zoezi hilo linalotarajiwa kuanza hivi karibuni la kuweka bendera nyekundu.

Hayo yamezunguzwa wilayani hapo wakati wa makabidhiano ya mradi wa nyumba za waganga katika kijiji cha kising’a na madarasa mawili katika kijiji cha Kimala.

Makabidhiano hayo yamefanywa rasmi na afisa mtendaji mkuu  wa kampuni ya New forest inayojishughulisha na kilimo cha miti na uzalishaji wa mazao ya misitu wilayani Kilolo, Tshepiso Dumasi aliyeahidi kuendelea kushirikiana na wananchi wa wilaya hiyo kutatua changamoto mbalimbali za kijamii hasa katika sekta ya elimu.

Zuma kujibu mashtaka ya rushwa Afrika Kusini
Klopp kuendeleza rekodi kumpiga Mourinho?