Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka maafisa wa wizara zilizo chini ya ofisi yake na wakuu wa mikoa kwenda katika viwanda vya uzalishaji Saruji kujua sababu za kupanda kwa bidhaa wakati serikali haijapandisha kodi, makaa ya mawe wala kufanya mabadiliko yoyote.

Akizungumza mbele ya Rais baada ya kuapishwa kuwa Waziri Mkuu katika viwanja vya Ikulu Chamwino Jijini Dodoma, Majaliwa amewataka maafisa hao kufikia Novemba 20, 2020 saa nne asubuhi, awe amepata maelezo ya kwanini bidhaa hiyo imepanda bei.

“Kuna upandaji wa Saruji bila sababu za msingi, miaka mitano iliyopita tulijenga mazingira ya biashara kuwa rahisi, hatukutarajia saruji kupanda, mheshimiwa Rais Magufuli naanza na hilo,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, amewashukuru wabunge wote kwa kuridhia jina lake kuwa Waziri Mkuu na kusisitiza kuwa tabia yake ni ilel ile ya kuwasikiliza na kuwahudumia kwa maslahi ya Taifa.

Miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Spika wa Bunge Job Ndugai na Jaji Mkuu wa Tanzania Professa Ibrahimu Juma.

Uundwaji serikali ya Libya bado kitendawili
Jafo aahidi makubwa endapo atateuliwa