Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama amehitimisha ziara yake nchini Tanzania ambayo ilikuwa ya mapumziko na kuelekea Kenya.

Msemaji wa Serikali ya Tanzania ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: “Rais Mstaafu wa Marekani @BarackObama amehitimisha mapumziko ya siku 8 pamoja na familia yake katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini.”

Katika picha zilizoambatanishwa na msemaji huyo zinaonesha Obama akisindikizwa uwanja wa ndege na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Dkt Augustine Mahiga

Obama alikuwa kwenye hifadhi ya taifa ya Serengeti kwa usiri mkubwa, ingawa ilifahamika kwamba angewasili nchini Kenya na kuhudhuria sherehe ya uzinduzi wa kituo kimoja cha hisani eneo alikozaliwa babake Kogelo, Siaya nchini Kenya.

Obama na wageni wake watahudhuria uzinduzi wa Sauti Kuu, Shirika lisilokuwa la kiserikali la kuwawezesha vijana lililoanzishwa na dadake wa kambo, Auma Obama katika eneo la Kogelo jimbo la Siaya siku ya Jumatatu.

Akiwasili nchini Kenya, Obama amelakiwa na Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wa Rais, William Ruto katika Ikulu ya Nairobi, ambapo ni ziara ya nne sasa ya Obama humo.

Obama amefanya ziara nchini Kenya mara tatu 1987, 1992 na 2015 wakati alipokuwa akihudumu kwa awamu ya pili ya urais na sasa mara ya nne na ya kwanza tangu aondoke madarakani Januari 20, 2017.

Imeelezwa kuwa, siku ya leo Jumatatu Julai 16, 2018 Obama anatarajiwa kuelekea Kisumu ambapo atapokelewa na Gavana wa mji huo, Anyang’ Nyong’o kabla ya kuelekea Siaya alikozaliwa baba yake katika kijiji cha Kogelo ambako ili kuzindua wakfu huo wa Sauti Kuu.

Wawakilishi, wasomi, viongozi wa dini na viongozi wa kijiji walikutana mjini Kogelo siku ya Ijumaa kujadiliana jinsi ya kumkaribisha Obama.

“Tulikuwa tukijadiliana kuhusu tutakavyomkaribisha. Pia tumejadiliana kuhusu mahitaji ya jamii ambayo tutataka kuwasilisha kwa Obama siku ya Jumatatu, Nicholas Rajula aliambia gazei la Daily Nation nchini Kenya.

”Tunataka kumkaribisha kijijini Kiafrika. Hii itafanyika iwapo kutakuwa na raia wengi kwa sababu hiyo tunataka kutoa ombi kwa waandalizi kumruhusu mwana wetu kuhutubia umma kwa ufupi, sio lazima katika eneo la hafla hiyo kwa kuwa ni dogo mno kuruhusu kila mtu kuingia.

Baada ya ziara yake nchini Kenya Obama ataelekea Afrika Kusini.

‘Dada’ mbaroni kwa kuiba kichanga cha Bosi
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 16, 2018