Rapa Henry Ohanga maarufu kama Octopizzo wa nchini Kenya, anatuhumiwa kumuua kijana mdogo aliyemkurupusha kutoka kwenye nyumba yake kama mwizi.

Familia ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 aliyetajwa kwa jina la Kenneth Abom imedai kuwa Octopizzo alimpiga kijana huyo kichwani na kitu chenye ncha kali baada ya kumkuta akiwa nyumbani kwake, na baadaye kijana huyo alijirusha kutoka ghorofa ya tatu na kupata majeraha mengine ambapo alifariki akiwa anapatiwa matibabu hospitalini.

Hata hivyo, Octopizzo amefanya mahojiano leo na KTN na kukanusha tuhuma hizo akidai kuwa kijana huyo aliingia bila ruhusa nyumbani kwake na kwamba baada ya kuzungumza naye aliachana naye lakini walipata taarifa baadaye kuwa amejirusha kutoka ghorofani.

“Hapana, mimi sikumpiga. Mtu wa kwanza kuongea naye baada ya tukio hilo ni baba yake. Sikujua ni kwanini alikuja nyumbani kwangu. Saa moja baadaye tulisikia huyo kijana amejirusha kutoka ghorofani,” alisema Octopizzo.

Akizungumza kwa niaba ya familia hiyo ambayo pia inayoishi katika makazi hayo aliyopo Octopizzo, kaka wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Paul Abom ameeleza kuwa mdogo wake alifika nyumbani akiwa ametapakaa damu zilizotoka kichwani, kabla ya kujirusha kutoka ghorofani.

“Alikuja nyumbani akiwa na jeraha na ametapakaa damu, aliingia bafuni akajisafisha lakini baadaye tukasikia amejirusha kupitia dirishani,” alisema Paul.

Ameeleza kuwa baada ya tukio hilo walimkimbiza katika hospitali iliyoko jirani na baadaye wakamhamishia Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Kenyatta ambapo alifariki.

Baba wa marehemu, Aggrey Abom pia amemkana Octopizzo akidai kuwa hakuzungumza naye kama alivyodai.

Aliongeza kuwa mtoto wake alikuwa anapenda kufanya muziki na hivyo huenda ndicho kilichomsogeza karibu na nyumba ya rapa huyo maarufu kutoka Kibera.

Majirani pia wameeleza kuwa walimuona Octopizzo akizozana na kumtimua kijana huyo kutoka nyumbani kwake lakini aliambiwa aache mara moja kwani naye pia anaishi kwenye makazi hayo (estate).

Familia ya marehemu imeeleza kuwa wanasubiri kupata majibu ya uchunguzi wa daktari yanayotarajiwa kutoka rasmi Jumatatu.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 22, 2019
Chukua hii: Rafiki wa Jay Z alivyojaribu kuchepuka na Beyonce, kilichompata

Comments

comments