Mkwaruzano wa kisiasa kati ya Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto na kiongozi wa ngome ya upinzani ya NASA, Raila Odinga umemuweka njia panda Rais Uhuru Kenyatta, imebainika.

Kenyatta hivi sasa anawahitaji wawili hao katika masuala mawili tofauti na muhimu kwa nchi hiyo. Anamhitaji Odinga kwa ajili ya kutuliza joto la kisiasa nchini humo huku akimuhitaji pia Ruto katika kusaidia kufanikisha utekelezaji wa Sera za nchi na ilani ya uchaguzi ya Jubilee.

Rais Kenyatta na Ruto waliunganisha nguvu kupambana na Odinga na kambi yake ya NASA, lakini mgogoro wa uchaguzi ulihitimishwa kwa Kenyatta kupatana na Odinga bila kumjulisha Ruto, hali iliyozua mijadala mingi.

Wiki hii, Ruto anayedaiwa kuwa na nafasi kubwa ya kugombea urais kwa tiketi ya Jubilee mwaka 2022, ametoa ya moyoni akidai kuwa tukio la kushikana mikono kati ya Kenyatta na Odinga sio tiketi ya kumsaidia kiongozi huyo wa NASA kutumia mbinu chafu dhidi yake.

“Tunajua nini maana ya kushikana mikono na tunajua pia wazi kuhusu ambacho sicho, kwahiyo haitupi mkanganyiko. Tukio la kushikana mikono sio leseni ya kuleta propaganda na ujanjaunja kwenye Jubilee yetu,” alisema Ruto.

Hata hivyo, kauli hizo za Ruto ziliibua taharuki na mijadala, ambapo viongozi wa NASA walijitokeza kuzilaani hadharani, wakidai kuwa anapaswa kumuomba radhi Odinga kwa kumuita ‘conman’.

Kati ya waliojitokeza ni pamoja na Hasan Joho, makamu kiongozi wa ODM.

“Inakuwaje unamuita Raila Odinga ‘conman’. Wewe una nini ya kuconiwa kwanza?,” alihoji.

Ingawa Odinga hajaweka wazi kama atagombea urais wa Kenya 2022, wafuasi wake wameendelea kuweka msimamo kuwa yeye ndiye atakayepeperusha bendera.

Rais Kenyatta sasa yuko kimya akitekeleza majukumu yake, huku akimhakikishia Odinga mazingira bora ya kufanya kazi yake ya kisiasa kama ilivyo kwa Ruto.

Madiwani wa CCM, Ukawa wapigana ngumi
Mbio za baiskeli kukusanya milioni 340

Comments

comments