Kampeni za uchaguzi wa Rais wa Marekani zimeingia dosari ya kiusalama baada ya ofisi moja ya chama cha Republican kilichomsimamisha Donald Trump, kuchomwa moto kwa bomu la kienyeji.

Maafisi wa Polisi wameeleza kuwa watu wasiofahamika walirusha chupa zilzojaa mafuta na kuziwasha moto katika ofisi ya chama hicho zilizopo ’Carolina Kaskazini’, na kuchoma baadhi ya vitu na nyaraka lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Watekelezaji wa tukio hilo ambao wanaonekana kuwa maadui wa chama hicho waliandika nembo na maandishi yanayopinga chama hicho.

Mkurugenzi wa Republican, Dallas Woodhouse alisema kuwa kutokana na tukio hilo baya, ofisi zote za chama hicho zimeelezwa kuchukua tahadhari ya kiusalama.

Trump amerusha lawama kwa chama cha Democratic akiwataja watekelezaji wa tukio hilo kama wanyama wanaomuwakilisha Hillary Clinton.

”Wanyama wanaomuwakilisha Hillary Clinton huko Carolina Kaskazini wamerusha bomu katika ofisi yetu kwa sababu tunashinda,” Trump aliandika kwenye Twitter.

Hata hivyo, Clinton kupitia akaunti yake ya Twitter, amelaani kitendo hicho na kueleza kuwa ni kitendo kisichokubalika.

Mbunge adaiwa kutafuna mishahara mitano ya utumishi hewa
Video: Magufuli aiunganisha familia ya Dk Masaburi