Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Augustine Okrah amesema amezoea kucheza michezo yenye hadhi ya Dabi, na hana wasiwasi na mpambano wa Kariakoo Dabi utakaounguruma kesho Jumamosi (Agosti 13) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Young Africans itacheza dhidi ya Simba SC kwa mara ya kwanza msimu wa 2022/23, ikitetea Ngao ya Jamii iliyoitwaa msimu uliopita kwa kumfunga Mnyama bao 1-0.

Kiungo huyo aliyesajiliwa Simba SC msimu huu akitokea Bechem United ya nchini kwao, amesema amekua mchezaji wenye uzoefu mkubwa wa michezo na namna hiyo, na anachokifanya sasa ni kumuomba Mungu ili aweze kuwa sehemu ya kikosi kitakachoikabili Young Africans Kwa Mkapa.

Amesema anatambua msimu uliopita haukuwa mzuri kwa Simba SC mbele ya Young Africans, lakini amewasini Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo kusahau yaliyopita, na badala yake waanze upya kuanzia kesho Jumamosi (Agosti 13).

“Haitakua Dabi yangu ya kwanza kucheza, nimekua mchezaji niliyezoea michezo ya aina hii, na nina hamu kubwa ya kuwepo kikosini dhidi ya Young Africans,”

“Kwa hapa Tanzania utakua mchezo wangu wa kwanza wa Dabi, lakini hakuna mchezo rahisi wenye hadhi ya Dabi popote pale duniani, Simba SC tumejiandaa vizuri na tumejiwekea mpango wa kupambana na kupata matokeo bora.”

“Simba hii ni tofauti kabisa na ile ya msimu uliopita, ni kama tunaanza upya, kwa hiyo yaliyotokea msimu uliopita yanapaswa kuwekwa pembeni, tunatakiwa kuangalia mchezo unafuata nani ataibuka na ushindi utakaompa taji la kwanza msimu huu.” amesema Okrah

Simba SC ina deni la kulipa kisasi cha kufungwa na Young Africans msimu uliopita, wakipoteza mchezo wa Ngao ya Jamii kwa 1-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, pia walikutana na matokeo hayo Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.

Kenya: Maafisa wa IEBC mikononi mwa Polisi
UN yasikitishwa na mauaji ya Watoto Gaza