Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Nigeria na Klabu ya Simba SC Nelson Okwa, amerejea nchini akitokea kwao Nigeria kwa ajili ya matibabu ya nyama za nyuma ya paja ambazo zilikuwa zikimsumbua.

Okwa aliumia kwenye mazoezi ya Simba siku moja kabla ya kucheza na Azam FC, mchezo ambao Simba ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0, ambalo lilifungwa na Prince Dube.

Baada ya kujitibia hapa nchini wiki moja na zaidi tangu alipopata maumivu Okwa aliuomba uongozi wa Simba wiki mbili za kwenda kwao Nigeria kwa ajili ya matibabu na uangalizi zaidi akiwa karibu na familia yake.

Katika matibabu hayo mambo yameonekana kuwa mazuri na asubuhi ya jana aliingia nchini akisubiri wenzake watoke Tanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara kesho Jumamosi dhidi ya Coastal, ili kujiunga nao kambini kwa ajili ya mazoezi na ratiba nyingine za timu.

“Nilienda nyumbani Nigeria kwa ajili ya kukaa karibu na familia na kupata huduma na matibabu mazuri kama niliyokuwa nikipatiwa Simba ila hapa nilikuwa naishi mwenyewe tofauti na nyumbani kuna watu wa karibu kunisaidia,” amesema Okwa aliyesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Rivers United ya kwao na kuongeza;

“Nashukuru Mungu maendeleo ni mazuri tofauti na ilivyokuwa hapo awali wakati nipo hapa nchini ambacho nasubiri wakati huu ni kujiunga na timu ili Daktari, aweze kuniangalia na kunieleza natakiwa kuanza na mazoezi gani,”

“Wakati nipo Nigeria nilikuwa nikiwasiliana na Daktari wa timu na alinielekeza vitu gani natakiwa kufanya akishirikiana na wale Madaktari wa kule, nashukuru Mungu maendeleo ni mazuri nimerudi nchini kwa ajili ya kujiunga na kikosi.”

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Decemba 3, 2022
Kisa Azam FC, Mshambuliaji Coastal Union afungiwa