Kocha wa Simba, Mrundi Masoud Djuma amesema amemsamehe Emmanuel Okwi baada ya kukosekana kikosini kwa muda mrefu bila sababu za msingi.

Akizungumza na katika dimba la Mzungu mjini Morogoro, kocha huyo amesema Okwi amerejea salama kikosini akiwa katika hali nzuri na kuomba radhi kwake, kwa uongozi, na wachezaji wenzake na jana alianza rasmi mazoezi na timu.

“Unajua binadamu hakuna aliyekamilika, cha lazima ni muunganiko wa pamoja, tukianza kunyoosheana vidole nguvu inapunguka, mimi kama mwalimu, mtu akishaomba msamaha, cha lazima ni kurudisha nidhamu kwenye timu. Hakuna mchezaji au mtu yeyote ambaye yuko juu ya timu, hata rais wa timu hayuko juu ya timu, timu inakuja kwanza halafu mtu baadaye,” amesema Masoud.

Kocha huyo ambaye anashikilia mikoba ya Joseph Omog aliyetimuliwa hivi karibuni ametumia nafasi hiyo kumuombea radhi Emanuel Okwi kwa mashabiki, akiwataka kuungana ili timu ifanye vizuri.

Kikosi cha Simba leo asubuhi kimeanza safari kurejea jijini Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa kesho dhidi Singida United utakaopigwa kwenye dimba la Taifa na kurushwa moja kwa moja na Azam TV kupitia channel ya Azam Sports 2.

Simba vs Singida Utd kuufungua uwanja wa Taifa
Nyumba ya katibu UVCCM yateketezwa na moto