Mshambuliaji wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, Emmanuel Okwi amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.

Okwi anayecheza nafasi ya ushambuliaji, alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Yahya Zayd wa Azam na Eliud Ambokile wa Mbeya City alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.

Kwa mwezi huo Oktoba timu 18 zilicheza michezo mitano kila moja,  isipokuwa Simba na Yanga zilizocheza mechi nne.

Katika michezo hiyo minne ambayo Simba ilicheza, Okwi raia wa Uganda alitoa mchango mkubwa kwa kupata pointi 12  kwa kushinda michezo yote na kumaliza ikiwa nafasi ya pili, huku Okwi akifunga mabao 7 kwa mwezi huo, matatu akifunga katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 5-0.

Kwa upande wa Ambokile naye alitoa mchango mkubwa kwa Mbeya City kufanikisha kupata pointi 11 baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare miwili na kushika nafasi ya nane katika msimamo, akifunga mabao manne.

Kuhusu Zayd alitoa mchango mkubwa kwa Azam akifunga mabao matatu katika michezo mitano ambayo Azam ilicheza ikishinda yote na kupata pointi 15 ikishika nafasi ya kwanza.

Pia Kamati ya Tuzo, imemchagua Kocha wa Azam FC, Han Pluijm kuwa Kocha Bora wa mwezi Oktoba akiwashinda Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems na Kocha Mkuu wa Mbeya City, Ramadhan Nsazwarimo.

Pluijm aliiongoza timu yake kupata pointi 15 baada ya kushinda michezo yote mitano iliyocheza na kushika nafasi ya kwanza, huku Aussems akiiongoza Simba kushinda michezo yote minne iliyocheza hivyo kupata pointi 12 na kushika nafasi ya pili, wakati Nsazwarimo alipata pointi 11 akishinda michezo mitatu na kutoka sare mitatu akiiwezesha timu yake kupanda hadi nafasi ya nane.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ina utaratibu wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2017/2018 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali, ambapo kwa ushindi huo Okwi atazawadiwa tuzo, king’amuzi kutoka Azam na Sh milioni moja kwa kuibuka Mchezaji Bora wa mwezi.

Washindi wengine wa tuzo hiyo kwa msimu huu na miezi yao katika mabano ni mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere na mshambuliaji wa Mbeya City Eliud Ambokile.

Kwa upande wa makocha walioshinda tuzo hizo kwa msimu huu ni Amri Said wa Mbao FC aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora wa Agosti na Mwinyi Zahera wa Yanga aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora wa Septemba.

Ikulu ya Marekani yafuta kibali cha mwandishi aliyejibizana na Trump
Kocha Michel Dussuyer kumtumia mzaliwa wa Ujerumani