Meneja wa Mashetani Wekundu (Manchester United) Ole Gunnar Solskjaer  amekingiwa kifuo na uongozi wa klabu hiyo, kwa kupea nafasi ya kuendelea kupanga mikakati yake ya muda mfupi na mrefu.

Solskjaer amekua katika wakati mgumu wa kulinda kibarua chake siku za karibuni, kufuatia msukumo mkubwa uliokua ukitolewa na mashabiki wa Manchester United, kutokana na matokeo hasiyoridhisha.

Meneja huyo kutoka nchini Norway ameshinda michezo mitano kati ya ishirini na tatu ya mwisho na kuifanya Manchester United kwa sasa kuwa alama mbili juu dhidi ya timu zilizopo kwenye shimo la kushuka daraja.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo yenye maskani yake Old Trafford imeeleza kuwa, uongozi unaelewa mipango ya meneja huyo, na hauangalii matokeo yaliyopatikana siku za karibuni.

Makamu mwenyekiti, Ed Woodward na wamiliki wa timu, familia ya Glazers kwa asilimia 100 wanamsapoti Solskjaer na hawatafanya mabadiliko yoyote ya benchi la ufundi, hata kama watafungwa na Liverpool kesho Jumapili.

Woodward, ambaye kauli yake inaonekana kama kijembe kwa mameneja waliopita baada ya kusema: “Ole amerudisha nidhamu kwenye timu kitu ambacho kilikosekana kwa miaka ya karibuni. Anajenga kikosi kitakachoheshimu historia ya klabu, huku wachezaji wakipambana na kuheshimiana wenyewe kwa wenyewe. Hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu.

“Mipango ya Ole ndio dira yetu kwa sasa. Lazima tushinde mataji, tucheze soka la kushambulia na kuwapa vijana nafasi. Katikati ya msimu uliopita, baada ya Ole kutua, alituonyesha mahali tunapotakiwa kwenda. Tumeona timu ikicheza soka la kasi na mtiririko mzuri.”

Video: Upepo wa kisulisuli ulivyozaa mjadala wa wasichana na ndoa
El Clasico kurindima Disemba 07