Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka amesema kuwa kauli zilizotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhusu Serikali ni za upotoshaji.

Hivi karibuni, Lowassa aliandika waraka wake kwa wananchi kuhusu mtazamo wake ikiwa ni mwaka mmoja tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ambao yeye alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na Ukawa, uchaguzi uliompa ushindi Rais John Magufuli (CCM).

Ole Sendeka amepinga kauli za Lowassa leo jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari ambapo amewataka wananchi kuzipuuza kauli hizo kwani Serikali ya Rais John Magufuli imefanya kazi kubwa inayotambulika hata nje ya mipaka ya nchi.

“Lowassa sio tishio mahali popote lakini huwezi kumuacha anazungumza jambo la kupotosha halafu ukasema jambo analozungumza Lowassa ni sawa na jambo linalozungumzwa na raia mwingine, hapana,” alisema Ole Sendeka.

Akizungumzia kauli ya Lowassa aliyoitoa kupitia waraka wake kuhusu mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu kuwa utumishi wa umma umekuwa kaa la moto, alisema inashangaza kwani wanachofanya ni kurejesha nidhamu ya utumishi.

“Tunaposhughulika kuhakikisha kwamba tunarejesha nidhamu kwa watumishi wa umma ambayo kwa kiasi fulani ilikuwa imetetereka, mwenzetu anasema ‘utumishi wa umma umekuwa kaa la moto’,” alisema.

Katika hatua nyingine, Msemaji huyo wa Serikali alisema kuwa vyama vya upinzani vimekuwa vikitengeneza matatizo miongoni mwao na baadae kuitumia lawama CCM.

Ole Sendeka pia ameishauri Serikali kuanza kukagua akaunti za wenyeviti wa Kamati za Bunge ili kuangalia miamala na fedha walizonazo kwa kulinganisha na kiasi cha mishahara yao. Lengo likiwa kubaini wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Meya wa CCM mbaroni kwa kuisababishia Serikali hasara ya Shilingi Milioni 226
Benki Kuu yachukua usimamizi wa Benki ya Twiga kuinusuru