Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amewaagiza viongozi wa serikali za mitaa wakiwemo wenyeviti wa vijiji kuhakikisha wanashiriki katika zoezi la kutoa taarifa za wahusika wa mauaji mkoani humo huku akiapa kuanza kushughulika na viongozi hao wa vijiji endapo yatatokea mauaji yanayofanana na yaliyotokea mkoani humo.

Ameyasema hayo akiwa katika mji mdogo wa Makambako mkoani humo wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa mji huo kwa lengo la kuwaomba wananchi kuonyesha ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama katika kushiriki kuwafichua wanaohusika katika mauaji ya watoto wadogo.

Amesema kuwa ameamua kusema hivyo kwasababu kumekuwepo na matukio yanayofanana na hayo katika kipindi cha nyuma ambapo watu wengi wamekuwa na ugomvi kuhusu mashamba huku wengine wakisingiziana ushirikina hivyo ni lazima watu wa namna hiyo wapatikane.

“Ninatarajia ninyi wachaguliwa mliopewa dhamana ya kuwa wenyeviti wa mitaa, wenyeviti wa vijiji, waheshimiwa madiwani mtoe ushirikiano wa kwanza kwa vyombo vyangu vya ulinzi na usalama juu ya haya niliyoyataja, kuanzia sasa hivi akifariki mtu mmoja kwenye mtaa wowote halafu mkatuambia ameuawa na watu wasiojulikana ninaanza na mwenyekiti wa mtaa huo, mwenyekiti wa kijiji hicho, mtendaji wa mtaa na wao wataunganishwa kwenye kesi ya mauaji,”amesema Ole Sendeka

Kwa upande wake kamishna mkuu wa oparesheni na mafunzo ya jeshi la polisi nchini Tanzania, Nsato Marijani ameendelea kusisitiza kulimaliza jambo hilo kwa hiari au kwa shari.

Nao baadhi ya wananchi mjini Makambako wamepongeza jitihada za serikali zinazoendelea huku wakiahidi kutoa ushirikiano kikamilifu kuwafichua waliohusika na mauji ya watoto sita (6) ili kumaliza tatizo hilo.

RC Songwe awashukia TBA kuhusu ujenzi wa nyumba za serikali
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 2, 2019

Comments

comments