Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Nigeria, Sunday Oliseh amelazimika kusafiri hadi nchini England kwa ajili ya kwenda kumshawishi mshambuliaji wa klabu ya Liverpool, Jordon Ashley Femi Ibe ili akubalia kurejea nyumbani na kuitumikia Super Eagles katika harakati za kuwania nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2017.

Ibe, kwa sasa anaitumikia timu ya taifa ya England chini ya umri wa miaka 20, na amekua muhimili mkubwa katika timu hiyo pamoja na klabu yake ya Liverpool ambayo imeanza kumtumia katika kikosi chake cha kwanza katika kipindi hiki cha kujianda ana msimu mpya wa ligi.

Oliseh amekwenda kufanya kazi hiyo ya ushawishi kwa Ibe, ikiwa ni sehemu ya shughuli ambayo alidhamiria kuifanya ya kukisuka upya kikosi cha Nigeria ambacho kilionekana kupoteza ladha ya ushindani barani Afrika kwa kipindi kirefu kilichopita.

Hata hivyo ushawishi wa kocha huyo mpya ambaye alikabidhiwa jukumu baada ya kutimuliwa kwa Steven Keshi, unatarajiwa kukabiliwa na mazingira magumu, kutokana na Ibe kuonyesha lengo la kujikita sana katika soka la barani Ulaya.

Oliseh anatarajia kuwa shuhuda wa mazoezi ya kikosi cha Liverpool hii leo  baada ya kufanya safari kutoka nchini Nigeria hapo jana na baada ya hapo atazungumza na viongozi wa Liverpool kwa kuomba ridhaa ya kukutana na mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 19.

Ibe alizaliwa kusini mwa jijini London nchini England,  Decemba 8 mwaka 1995 na mzazi wake wa kiume ni raia wa nchini  Nigeria hivyo ana nafasi ya kukubaliana na ombi la Oliseh la kurejea nyumbani na kuitumikia Super Eagles.

Nigeria watapambana na Tanzania katika mchezo wa kuwania kucheza fainali za Afrika za mwaka 2017, katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam Septemba 05 mwaka huu.

Crystal Palace Wainasa Saini Ya Sako
Siri Ya De Gea Kuihama Man Utd Yafichuka