Mahakama Kuu Dar es Salaam, imetupa maombi ya Halima Mdee na wenzake 19, ya kupata kibali cha kupinga kufukuzwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kutokana na kasoro za jina zilizojitokeza.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA), na wenzake waliwekewa pingamizi na jopo la mawakili wa CHADEMA likiongozwa na Peter Kibatala, wakiiomba Mahakama isiyasikilize maombi yao wakidai yana kasoro za kisheria kwa kubainisha hoja sita.

Wajibu wa maombi ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambapo uamuzi wa leo ulitarajiwa kutoa hatima ya usikilizwaji wa maombi ya kina Mdee ya kupewa kibali kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama wao.

Kwa uamizi huu ni wazi kuwa Mahakama imekubaliana na hoja za pingamizi la Chadema, ingawa haimaanishi imewafungia milango kwani wana fursa ya kuyafungua upya baada ya kurekebisha kasoro ambazo zimeainishwa.

Mbali na Halima waliopo katika kesi hiyo ni Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnes Lambart, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed na Felister Njau.

Wengine ni Naghenjwa Kaboyoka, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Rwamlaza na Sophia Mwakagenda.

Meya wa jiji, watendaji wake wasimamishwa kazi
Wajane waomba sheria za mirathi zifanyiwe mabadiliko