Wakati Chama Cha Wananchi (CUF) kikiwa katika vuguvugu la kudai kuundwa kwa serikali ya mpito visiwani Zanzibar kutokana na kutokubaliana na kufanyika kwa uchaguzi wa marudio na matokeo yake, jana suala la kukifuta chama hicho lilisikika bungeni.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Munira Mustafa Khatib, jana aliihoji Serikali kuwa kwanini isichukue hatua ya kukifuta chama hicho kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar kwa madai kuwa kimekuwa chanzo kikuu cha vurugu zinazopelekea uharibifu wa mali za wananchi hususan visiwani Pemba.

Mbunge mwingine wa viti maalum (CCM), Tauhida Cassian Nyimbo alitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya viongozi wa CUF ambao alidai wanatoa kauli za kichochezi na kusababisha kuwepo kwa matukio hayo.

Maswali hayo pia yalimvuta Mbunge wa Chambani (CUF), Yusufu Salim Hussein ambaye alitaka Serikali kueleza kama inatambua uwepo wa vitendo vya wananchi kupigwa na kuharibiwa mali zao visiwani Zanzibar na hatua inazochukua.

Akitoa majibu ya maswali hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, alisema kuwa Serikali haina mamlaka ya kukifuta chama chochote cha siasa kwani hilo ni jukumu la kisheria la Msajili wa vyama vya siasa nchini.

Naibu waziri huyo aliongeza kuwa Serikali inatambua uwepo wa matukio ya vurugu na uharibifu wa mali kila baada ya uchaguzi mkuu visiwani humo na kwamba itawachukulia hatua wote wanaohusika bila kujali nyadhifa zao.

“Hakuna mtu ambaye yuko juu ya sharia. Wale watakaoleta ukorofi watachukuliwa hatua kali bila kujali kama ni kiongozi wa aina gani na mahali gani anatokea. Lazima sheria ichukue mkondo wake,” alisema.

Aliwahakikishia wananchi kuwa nchi iko salama na kwamba hakuna Serikali itaendelea kuhakikisha kuna utulivu na amani wakati wote nchini.

Video: Rais Magufuli amewaapisha wakuu wanne wapya wa mikoa
Rais Magufuli Atoa Sababu Ya Utenguzi Wa Mkuu Wa Wilaya Ya Ikungi