Ommy Dimpoz ambaye alifanyiwa upasuaji wa koo nchini Ujerumani, ameweka wazi baadhi ya jumbe za watu mbalimbali ambazo zilimuumiza na kumkera alipokuwa anaendelea na matibabu.

Mwimbaji huyo wa ‘Ni wewe’ amesema kuwa kutokana na baadhi ya watu kukariri kuwa maisha ni lazima yawekwe kwenye Instagram, walikuwa wakimtumia jumbe ambazo zilimhoji kuhusu masuala ambayo hawana uhakika nayo.

Akizungumza wiki hii na The Playlist ya Times Fm, Ommy Dimpoz alisema kuwa alikerwa na mtu mmoja alimuandikia ujumbe akimhoji kuwa kwanini hakumpa pole Ali Kiba kwa kufiwa na baba yake.

“Kuna mtu aliniandikia akaniambia mbona hujampa pole Ali Kiba kwa kufiwa na baba yake… hey common, kivipi? Wewe unajuaje? Kwanini maisha tuyageuze kuwa matangazo? Unamridhisha nani?” Alihoji na kufafanua kuwa watu wanasahau kuna maisha nje ya mitandao ya kijamii.

Msanii huyo ambaye ujio wake wa wimbo uliokuwa gumzo kubwa wiki hii, alitoa mfano mwingine wa alichokiona kwenye mitandao ya kijamii ambapo kuna watu walikuwa wanamhoji Christian Bella wakidai hajaenda kumsalimia hospitalini licha ya kuimba naye wimbo ‘Nani Kama Mama’.

Lakini wameyapata majibu baada ya kusikia wimbo mpya wa Ommy akiwemo Christian Bella, wimbo waliourekodi akiwa anaendelea na matibabu.

Katika hatua nyingine, mwanafamilia huyo wa Rockstar Africa alisema kuwa hivi karibuni akiwa jijini Dar es Salaam alisoma ujumbe wa mtumiaji mmoja wa mitandao ya kijamii uliomuumiza na kumshangaza.

“Nilichukua tu simu, kwa bahati mbaya naangalia comments, mtu kaandika ‘aah hii video ina mishumaa yaani huyu mbwa hajafa hadi leo!’ Imagine ni mtu anakuwandikia hivyo,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuwa wapo watu wengi ambao walimuandikia jumbe nyingi za kumpa moyo na zilizomuongezea nguvu.

Kwa mujibu wa madaktari wake, chanzo cha tatizo lake la koo ni kula sumu ambayo ilimdhuru.

 

Solskjaer aweka wazi mtihani aliopewa na Bodi ya Man Utd
Milioni 451 kuboresha Elimu Wilayani Mtwara

Comments

comments