Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa Ofisi yake waongeze kasi ya utendaji ili utendaji kazi serikalini uweze kufikia hatua nzuri.

Ameyasema hayo jijini Dodoma alipokutana na viongozi na watumishi wa ofisi yake na kufuturu nao pamoja kwenye makazi yake jijini humo.

“Ninawashukuru watumishi wote kwa ushirikiano mnaotupatia mimi pamoja na mawaziri wenzangu, makatibu wakuu wote watatu, Wakurugenzi mbalimbali na wakuu wa vitengo. Tunatakiwa tuongeze kasi ili tufikie hatua nzuri ya utendaji kazi serikalini,”amesema Majaliwa

Aidha amesema kuwa utendaji kazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu ni mgumu kwa sababu unahusika na usimamizi wa shughuli za Serikali nzima na watendaji wote wa Serikali.

“Sekta yetu ni ngumu kwa sababu sisi ni wasimamizi wa Serikali na watendaji wote wa Serikali. Tuna wajibu wa kuwaunganisha watendaji wa wizara zote serikalini,”ameongeza Waziri Mkuu.

Hata hivyo, ameongeza kuwa wao wote ni watumishi wa umma, kwa hiyo mchango wao una maana kubwa na unachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Serikali nzima kwa ujumla, hivyo amewapongeza kwa utumishi mwema na wenye uadilifu.

Video: RC Makonda awatangazia kiama wafanyabiashara ndogo ndogo
Nyalandu ashikiliwa tena na polisi, atoka kwa dhamana