Operesheni ya kukata maji kwa wateja ambao wamegeuka kuwa wadeni sugu, haiachi jiwe juu ya jiwe. Hii imethibitishwa baada ya kutua nyumbani kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Ramadhani Mungi  na baadhi ya taasisi nyeti za serikali.

Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Moshi (Muwsa) jana ilithibitisha kuwa imezikatia maji taasisi tatu nyeti za serikali likiwemo eneo la kambi za polisi na makazi ya Kamanda wa jeshi hilo kutokana na malimbikizo ya madeni ya zaidi ya shilingi bilioni 1.3.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa, Joyce Msiru

Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa, Joyce Msiru

Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa, Joyce Msiru alieleza kuwa hadi kufikia jana majira ya saa nne tayari walikuwa wamezikatia maji taasisi hizo na maeneo tajwa. Alifafanua kuwa Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro inadaiwa shilini milioni 528.6, Chuo cha Mafunzo ya Polisi kinadaiwa shilingi milioni 401.9 na Magereza shilingi milioni 203.7.

Hata hivyo, Kamanda Mungi alipopigiwa simu na mwandishi wa habari jana alieleza kuwa alikuwa mbali na makazi yake na kwamba hajapata taarifa kuhusu kukatwa maji.

Afisa Mnadhimu wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa askari wa jeshi hilo kuhusu katizo la huduma ya maji.

“Nimepata malalamiko kutoka kwa askari kuwa kambini hakuna maji. Ndio nafuatilia hapa kujua tatizo liko wapi,” Moita anakaririwa.

Polisi yawasaka wamiliki na wahariri wa Gazeti la 'Mawio'
Wananchi wauziana shamba la Sumaye, Sumaye mwenyewe azungumza