Jarida la Forbes limetoa orodha mpya ya mabilionea wa Afrika walioweza kubaki kwenye ubilionea wao na walioweza kuufikia ubilionea hadi Januari 2019.

Kupitia orodha hiyo, raia wa Nigeria, Aliko Dangote ameendelea kukaa kileleni akiwa na utajiri wa $10.3 bilioni, ambazo hata hivyo ni pungufu kwa $2 bilioni za mwaka jana. Chanzo cha kupungua kwa utajiri wa Dangote mwenye umri wa miaka 61 kimetajwa kuwa ni kushuka kwa hisa za biashara yake ya Saruji kwa asilimia 20.

Aliko Dangote

Nafasi ya pili imerudi kwa raia mwingine wa Nigeria, Mike Adenuga mwenye utajiri wa $9.2 bilioni. Tofauti na Dangote, kiwango cha utajiri wa Adenuga kimepanda kutoka $5bilioni za Januari 2018. Bilionea huyu anamiliki kampuni ya Simu ya Globacom, inayoshika nafasi ya tatu nchini Nigeria. Pia, anamiliki kampuni inayofanya biashara ya mafuta pamoja na makampuni mengine makubwa.

Nicky Oppenheimer, raia wa Afrika Kusini ameshika nafasi ya tatu katika orodha ya mwaka huu. Utajiri wake umethaminishwa kuwa ni $7.3 bilioni, ikiwa umeshuka kutoka $7.7 za mwaka jana. Alijipatia utajiri mkubwa baada ya kuuza kampuni ya kuchimba madini ya almasi ya DeBeers mwaka 2012. Aliiuza kampuni hiyo iliyoasisiwa na babu yake kwa $5.1 bilioni alizolipwa taslimu.

Katika orodha hiyo ndefu ambayo imeshuhudia kupungua kwa mabilionea watatu kwa kulinganisha na orodha yam waka jana, Mtanzania pekee, Mohammed Dewji maarufu kama Mo Dewji ametajwa kwenye nafasi ya 14 akiwa na utajiri wa $1.9 bilioni.

Mo Dewji ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya METL ambayo yaliasisiwa na babu yake mwaka 1970, amebakiza dola kadhaa afikishe utajiri wa $2bilioni. Makampuni ya METL yapo katika nchi sita barani Afrika. Mwaka 2016, aliweka ahadi ya kutoa takribani nusu ya utajiri wake kuhakikisha inasaidia jamii.

Katika orodha hiyo pia kuna wanawake wawili tu, Isabel dos Santos ($2.3 bilioni) akishika nafasi ya nane. Isabel ni mtoto wa rais wa zamani wa Angola, Jose Eduardo dos Santos. Anamiliki hisa za makampuni kadhaa makubwa nchini Uholanzi ikiwa ni pamoja na kampuni ya Televisheni ya Nos SGPS.

Mwanamke mwingine bilionea ni Folorunsho Alakija ($1.1 bilioni) ambaye ni raia wa Nigeria na Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Famfa Oil inayofanya kazi ya kuchimba mafuta nchini humo.

Bofya hapa kuona orodha kamili

Picha: Huddah atimba mtaani na buibui kusaka matapeli
Serikali: Marufuku shule binafsi kufukuza wanafunzi kisa ada