Klabu ya SSC Napoli huenda ikasitisha mpango wa kumsajili mlinda mlango kutoka nchini Ubelgiji na Liverpool Simon Mignolet, baada ya kuthibitisha kumfanyia tathmini ya kina David Ospina wa Arsenal.

Rais wa klabu hiyo ya mjini Naples-Italia Aurelio de Laurentiis, amesema pamoja na tarifa za uwezekano wa Mignolet kutolewa jana katika vyombo vya habari duniani kote, wameona kuna ulazima wa kufanya tathmini ya mlinda mwingine kutoka Arsenal ili kujiridhisha ni nani anastahili kusajiliwa klabuni hapo.

Ospina yupo kwenye harakati za kutaka kuihama Arsenal kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi mwishoni mwa mwezi huu, kufuatia hatua ya kusajiliwa kwa mlinda mlango kutoka nchini Ujerumani Bernd Leno.

Tayari alikua anahusishwa na mipango ya kusajiliwa na klabu ya Besiktas ya Uturuki, lakini mazungumzo dhidi ya Arsenal yanadaiwa kuvunjika kutokana na ada ya uhamisho wake iliyotaka kulipwa kutofikia kiwango kinachotakiwa huko kaskazini mwa jijini London.

De Laurentiis aliambia Radio Kiss Kiss ya mjini Napoli: “Mpaka sasa tuna watathmini walinda mlango watano Ochoa, Mignolet, Ospina, Ciprian Tatarusanu na Simon Mignolet.

“Yoyote kati ya hawa atakaekidhi vigezo tunavyo vikusudia tutamsajili kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili mwishoni mwa mwezi huu”

“Hata hivyo mpaka sasa Ospina anaonyesha kuwa katika mipango yetu kutokana na kuwa na asilimia kubwa ya vigezo tunavyo vihitaji.”

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 29, alijiunga na Arsenal akitokea Nice ya Ufaransa, baada ya kufanya vizuri katika fainali za kombe la dunia mwaka 2014.

Mara ya mwisho kukaa langoni mwa The Gunners ilikua mwezi Februari mwaka huu, wakati wa mchezo wa fainali ya kombe la ligi nchini England chini ya utawala wa Arsene Wenger, ambapo Arsenal walikubali kibano cha mabo matatu kwa sifuri kilichotolewa na Man City.

Awali alikua chaguo la pili baada ya Petr Cech, lakini anaamini kusajiliwa kwa Bernd Leno ataendelea kushushwa zaidi, na kuwa mlinda mlango chaguo la tatu wa klabu ya Arsenal.

Majaliwa aagiza kukamatwa kwa Mtendaji
Utafiti wa LHRC wabaini wafanyakazi wengi hawazijui haki zao