Kiungo kutoka nchini Ujerumani na klabu ya Arsenal, Mesut Ozil amekanusha taarifa zilizodai kwamba huenda akaondoka kaskazini mwa jijini London (Emirates Stadium) mwishoni mwa msimu huu, endapo meneja Arsene Wenger ataendelea kusalia klabuni hapo.

Taarifa hizo zilitolewa mwanzoni mwa juma hili na jarida la michezo la nchini Hispania liitwalo Don Balon, kwa kudai kiungo huyo amechoshwa na mwenendo wa Wenger ambao umekua hauleti tija ya kusaka mafanikio.

Ozil, amedai kwamba taarifa zilizochapishwa na jarida hilo dhidi yake, zina lengo la uchochezi ambao haupaswi kufumbiwa macho, hasa katika kipindi hiki ambacho wachezaji wa Arsenal, wanahangaikia namna ya kusaka ubingwa wa nchini England.

Kama hiyo haitoshi, Ozil aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter “Mmeona taarifa iliyotolewa dhidi yangu. Arsene Wenger alikua sababu kubwa kwangu kujiunga na klabu ya Arsenal – na hii katu haitobadilika! #Heshima #AFC”

Ozil, alijiunga na Arsenal akitokea Real Madrid mwaka 2013, kwa ada ya uhamisho wa paund million 42.5, na tayari wameshafunga mabao 19 katika michezo 109 aliyocheza.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27, amekua na mwenendo mzuri kwa msimu huu, baada ya kufunga mabao saba katika michezo 38 mpaka sasa.

Wenger amekua akipokea changamoto kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa Arsenal, ambao wanamtaka aiache klabu hiyo itakapofika mwishoni mwa msimu huu, kutokana na kushindwa kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa nchini England, kwa kipindi cha miaka 12.

Kwa sasa Arsenal, wapo nyuma kwa point 11, dhidi ya vinara wa ligi ya nchini humo, Leicester City, huku michezo minane ikisalia kabla ya msimu wa 2015-16 haujafikia kikomo mnwezi May mwaka huu.

Andy Murray Ampinga Novak Djokovic
Timu Ya Ferrari Yapata Msiba