Kocha Mpya wa Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC Pablo Franco Martin amefunguka kwa mara ya kwanza tangu alipotangazwa kuwa kinara kwa walioomba kazi ndani ya klabu hiyo.

Pablo alitangazwa kushinda nafasi ya kuwa Kocha Mkuu Simba SC Jumamosi (Novemba 06) majira ya usiku, baada ya kutimiza vigezo vilivyokua vinatakiwa na jopo maalum lililopewa kazi ya kumsaka kocha mpya wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika mashariki na kati.

Simba ilianza mchakato wa kumsaka kocha mpya, baada ya kuachana na Didier Gomes, kufuatia kushindwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2021/22.

Kocha huyo amefunguka kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram akiandika: Ningependa kuawashukuru Mashabiki wote wa klabu ya Simba SC, kwa mapenzi amkubwa mlionionyesha, Ninawaahidi tutafanya kazi kwa pamoja hivyo tunaweza kuleta mabadiliko kwenye timu yetu na kushinda mataji Zaidi, ASANTENI SANA.

Pablo aliyekuwa akiinoa klabu ya Ligi Kuu ya Kuwait ya Al-Qadsia anakuja nchini akiwavutia mabosi wa Msimbazi kwa sifa zake zinazolingana kwa kiasi kikubwa na alizokuwa nazo kocha wao wa zamani, Sven Vandenbroeck aliyewafikisha kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu uliopita kisha kutimkia FAR Rabat ya Morocco.

Taarifa zinasema kuwa kocha Pablo huenda akatambulishwa kesho jumanne mbele ya waandishi habari ili kuwawatumikia mabingwa hao wa Bara ambao pia ni wawakilishi pekee wa nchi katika michuano ya kimataifa, ikiwa inashiriki mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mguto aibuka sakata la GSM
CHADEMA kutoshiriki uchaguzi mdogo wa Ngorongoro