Promota mkongwe wa mchezo wa masumbwi duniani, Bob Arum ameeleza hofu yake kuwa huenda Manny Pacquiao akapata majeraha ya ubongo katika pambano lake lijalo dhidi ya Keith Thurman jijini Las Vegas nchini Marekani.

Arum mwenye umri wa miaka 87, amesema kuwa hofu yake ni kwamba kutokana na umri wa Pacquiao (41) kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa kuhimili kipigo kitakachotolewa na Thurman ambaye ana umri wa miaka 30 na hajawahi kupoteza pambano hata moja.

Promota huyo mkongwe amewahi kufanya kazi na Muhammad Ali na pia amewahi kufanya kazi kwa muda mrefu na Pacquiao kupitia kampuni yake ya ‘Top Rank’.

Akizungumza jana kwenye mkutano na waandishi wa habari uliolenga kulitangaza pambano litakalofanyika leo kati ya Tyson Fury na Tom Schwarz, Arum alisema kuwa anampenda sana Pacquiao na ndio sababu anajaribu kumtahadharisha asipate majeraha kama aliyoyapa hivi karibuni mpiganaji mkongwe, Zab Judah (41) aliyelazwa muda mfupi baada ya pambano lake.

“Angalia, nampenda sana Manny Pacquiao, nina historia nzuri naye lakini nimekuja kubaini kuwa ana umri wa miaka 41… na wapiganaji wanapofikia umri kama huo ni bora waache, hataweza kufanya vizuri kama alivyokuwa na umri wa miaka 30,” alisema Arum.

“Madaktari watakwambia, unapokuwa na umri mkubwa sana ubongo unakuwa hauna kinga nzuri kama ulivyokuwa kijana. Kwahiyo, ukipigwa ngumi nzito inapenya kirahisi na inaweza kuleta majeraha,” aliongeza.

Alisema uwezo wa Keith Thurman wa kupiga makombora mazito unajulikana na kwamba huenda yakamuelemea mpiganaji huyo ambaye ni Seneta nchini kwake.

Keith ametangaza kuwa atampa kipigo kikali Pacquiao na kumfanya aachane kabisa na mchezo wa masumbwi kwakuwa anaona hataki kufuata nyayo za mkongwe mwenzake, Floyd Mayweather za kustaafu kwa hiari.

Hata hivyo, Pacquiao ameahidi kumpasua Thurman na kumfanya ale maneno yake mwenyewe akiwa ulingoni.

Pambano ni Julai 20 mwaka huu, Muda utatoa majibu sahihi.

Ali Kiba afunguka wasanii Bongo kutotajwa Tuzo za BET 2019
Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro yanufaika na Kilimo cha Umwagiliaji

Comments

comments