Bingwa wa zamani wa dunia wa masumbwi, Manny Pacquiao amekataa pambano lililokuwa linaandaliwa na promota wake, Bob Arum.

Bob Arum amekuwa akitangaza kuwa Pacquiao atapanda ulingoni nchini Marekani Aprili 14 dhidi ya Mike Alvarado na kwamba pambano hilo litakuwa la kusindikiza pambano kati ya Jeff Horn na Terrence Crawford ambao watapambana usiku huohuo.

Kwa kuzingatia kuwa Pacquiao ambaye ni nguli aliyekwishapambana na Jeff Horn na kupoteza pambano hilo nchini Australia huku akidai kuwa alipokonywa ushindi kwa njama, kambi yake imedai kuwa tangazo la pambano hilo la kusindikiza lilikuwa kama matusi kwake.

“Hapana, Pacquiao hatapigana siku hiyo. Amekataa uamuzi wa Bob Arum kumpanga kuwa msindikizaji wa pambano kati ya Jeff Horn na Terrence Crawford,” Afisa Mahusiano wa Pacquiao, Aquiles Zonio alisema.

“Hayo ni kama matusi kwa Pacquiao. Dunia nzima inafahamu nani alishinda pambano chafu kati ya Jeff na Pacquiao nchini Australia,” aliongeza.

Aidha, Pacquiao amekataa kupigana na Alvarado ambaye yuko chini ya kampuni ya Top Rank ya Bob Arum, na amemchagua bingwa wa masumbwi ambaye yuko chini ya kampuni hasimu kwa Bob Arum inayoongozwa na bingwa wa zamani wa masumbwi, Oscar Delahoya ya Golden Boy Entertainment.

Video: Deontay Wilder amshikisha adabu Ortiz, amvimbia Anthony Joshua
Marekani yaingilia mgogoro wa kisiasa Ethiopia