Zikiwa zimebaki saa chache dunia ishuhudie pambano kati ya aliyekuwa bingwa wa dunia bila kupoteza pambano, Floyd Mayweather na bingwa wa mapigano ya masumbwi na mieleka, Conor McGregor, bondia Mfilipino, Many Pacquiao ameungana mashabiki wa Mayweather.

Pacquiao ambaye alipoteza katika pambano lake na Mayweather mwaka 2015, pambano lililopewa jina la ‘Pambano la Karne’ amesisitiza kuwa McGregor hataweza hata kufikisha ngumi moja ya maana kwa Mayweather.

“McGregor hana namna yoyote ambayo ataweza kufikisha ngumi ya maana kwa Floyd. Hivi atawezaje? Alihoji. “Hana ujuzi na weledi wa mchezo wa masumbwi,” aliiambia Yahoo.

Hata hivyo, Pacquiao alienda mbali na kueleza kuwa pambano hilo litakuwa bovu na huenda likawa ‘linaboa’ (boring). Aliendelea kulipigia chapuo pambano kati ya Gennady Golovkin maarufu kama GGG na Canelo Alvarez litakalofanyika mwezi Septemba mwaka huu.

“Pambano la kweli ni Golovkin Vs Canelo. Pambano la bondia bora dhidi ya bondia bora. Na hilo ndilo pambano nitakaloangalia,” alisema.

Kwa upande wa ‘GGG’, alipoulizwa kuhusu pambano la FloydMcGregor alionesha kulishusha kama pambano la masumbwi na kuliita tukio kubwa la kibiashara.

Hata hivyo, aliyekuwa bingwa wa masumbwi uzito wa juu ambaye hajawahi kupoteza pambano, Tysona Fury aliweka karata yake kwa McGregor akidai kuwa atamzimisha Mayweather katika raundi ya kwanza tu ya pambano hilo.

Pambano hilo litakalofanyika kesho alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki linatajwa kuwa huenda likavunja rekodi ya mapato iliyowekwa na pambano la Mayweather na Pacquiao mwaka 2015.

Hata mimi siwatambui akina Seif- Ndugai
Ofisi za IMMMA Advocates zateketea kwa moto