Bingwa wa dunia wa masumbwi ya uzito wa welterweight, Manny Pacquiao anatarajia kupigana na Andrien Broaner ambaye ni swahiba mkubwa wa Floyd Mayweather.

Pambano hilo litakuwa pambano la kukaribisha pambano la marudiano kati ya Pacquiao na Mayweather ambalo wawili hao walithibitisha wiki kadhaa zilizopita.

Broner ambaye mbali na kutajwa kama bondia ngangari awapo jukwaani, anapewa sifa nyingi za kujua kutumia vyema mdomo wake kuuza mapambano yake hasa anavyotamba dhidi ya wapinzani wake.

Kwa mujibu wa ratiba ya ukumbi wa MGM Grand wa Las Vegas nchini Marekani, pambano hilo litafanyika kati ya Januari 12 na 16 mwakani.

Katika moja ya mapambano yake ya mwisho, Broner alitoa sare na Jessie Vargas Aprili mwaka huu, bondia ambaye aliwahi kupoteza dhidi ya Pacquiao.

“Ninachoahidi ni kwamba nitafanya kazi yangu vizuri na nitamrudisha Ufilipino akawe Gavana,” Broner ametamba.

Pacquiao ambaye ni Seneta nchini kwake, anatajwa kuwa chaguo la rais wa nchi hiyo kugombea urais kwa tiketi ya chama tawala miaka michache ijayo.

Wakati Pacquiao akijiandaa na pambano dhidi ya Broner, Mayweather anatarajia kupigana jijini Tokyo nchini Japan kama sehemu ya pambano la kurejea na kujiandaa na pambano dhidi ya Pacman.

Mayweather na Pacquiao wanatarajia kupambana mapema mwakani.

CCTV kamera zawaumbua makachero wa S. Arabia mauaji ya mwandishi
Lema aeleza alichoulizwa Polisi kuhusu Mo Dewji kutekwa

Comments

comments