Padri wa Kanisa Katoliki, Dayosisi ya Bungoma nchini Kenya amefariki dunia baada ya kuanguka akiwa anatoa huduma madhabahuni.

Kwa Mujibu wa Askofu Kong’oo Wambua wa jimbo la Bungoma, Padri James Mabele alianguka wakati akitoa huduma madhabahuni jana majira ya saa kumi jioni katika kanisa la Mabanga na alipoteza maisha dakika chache baadaye.

Padri Mabele ameripotiwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa ini kwa muda mrefu na kwamba huenda ikawa ndio chanzo cha kifo chake.

Mwili wake bado uko kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya Bungoma ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.

Askofu Wambua ameiambia Citizen ya Kenya kuwa mipango ya mazishi ya padri huyo inaendelea na kwamba atazikwa Bungoma.

“Natoa pole kwa familia ya Marehemu Mabele pamoja na kanisa. Alikuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa watu wengi alipokuwa akifanya kazi ya kanisa kwa miaka 38,” alisema Askofu Wabua.

Video: Mgunduzi Tanzanite alivyolala milionea, Magufuli aahidi neema kwa vijana 2,000 JKT
Majambazi walipua na kupora benki tano