Klabu ya Valencia CF imetangaza kumtimua meneja Pako Ayesteran kufuatia mwenendo wa kikosi chao kuwa mbaya tangu walipoanza msimu wa 2016/17.

Valencia CF wamefanya maamuzi ya kumtimua Ayesteran baada ya miezi sita kupita tangu walipomtangaza kuwa mkuu wa benchi la ufundi badala ya Gary Neville aliyetimuliwa mwishoni mwa msimu uliopita.

Valencia CF ipo mkiani mwa msimamo wa ligi ya nchini Hispania (La Liga) na mpaka sasa hawajapata point yoyote katika michezo minne waliyocheza.

Mwishoni mwa juma lililopita walipoteza kwa kufungwa mabao mawili kwa moja dhidi ya Athletic Bilbao, hatua ambayo iliongeza chachu kwa viongozi kuafiki maamuzi ya kumtimua meneja huyo kutoka nchini Hispania.

“Valencia Club de Fútbol imefikia maamuzi ya kuachana na meneja Pako Ayestarán. Na maamuzi haya yamefanyika baada ya kumfanyia tathmini ya kina na kuonekana hatoweza kufikia lengo la msimu huu.” Imeeleza taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Valencia CF.

Ayesteran anakua meneja wanane kutimuliwa na uongozi wa klabu hiyo, tangu mwaka 2012.

Kufuatia maamuzi hayo, kocha wa kikosi cha wakubwa klabuni hapo Salvador Gonzalez (Voro) ameteuliwa kuwa meneja wa muda, hadi hapo uongozi wa Valancia CF utakapompata mkuu wa benchi la ufundi.

Mchezaji Bora Wa Dunia Atapatikana Kwa Mfumo Huu
Cesc Fabregas: Nimewaziba Midomo Waandishi Wa Habari