Afya ya wakazi wa jiji la Dar es salaam ipo hatarini kufuatia mtindo uliozuka na wapishi wa supu ya utumbo unaotumia dawa ya kutuliza maumivu ya panado, kilevi cha konyagi pamoja na maziwa kupikia supu iyo kwa lengo la kuifanya ilainike na iive mapema ili kuondokana na matumizi makubwa ya kuni, mkaa na gesi.

Mwajuma ambaye ni mama lishe amesema kuwa vidonge vya panado pamoja na maziwa hutumika kulainisha utumbo, konyagi kutoa shombo na kwamba viungo hivyo hufanya supu iwe na ladha nzuri iliyochanganyika na uchachu ambao unawavutia wateja wengi.

”Tunatumia vidonge aina ya panado kulainisha nyama, huku kilevi aina ya konyagi kikitumika kuondoa harufu au shombo ya utumbo na maziwa kulainisha utumbo wenyewe kwa kuwa unapowekwa konyagi lazima uchanganye na maziwa ili utumbo ulainike zaidi” amesema Mwajuma.

Gazeti la Jamvi la habari limefanya uchunguzi huo na kubaini hayo ambapo waliweza kuzungumza na mama ntilie aliyefahamika kwa jina la Mwajuma aliyetoa maelezo hayo na kuongeza kuwa upishi huo kwa sasa ni jambo la kawaida na unafanywa na watu wengi.

Amesema kikawaida utumbo huchukua saa mbili hadi tatu kuiva lakini walipogundua njia hiyo utumbo unatumia saa moja kuiva na kuwa mlaini ambapo idadi ya vidonge vinavyotumika hutegemea na wingi wa utumbo lakini unaweza kuweka vidonge vinne hadi vitano huku konyagi huwekwa kwa kipimo kidogo kimoja au viwili.

Gazeti hilo lilifanya jitihada za kuongea na Afisa Afya wa jijini Dar es salaam, Enezaeli Ayo ambaye  amesema kuwa upishi wa kuweka konyagi na vidonge si upishi mzuri na haukubaliki kiafya kutokana na madhara mengi yanaoweza kutokana na mchanganyiko huo.

Ametaja mtumiaji wa supu yenye mchanganyiko huo ana hatari ya kupata magonjwa kama vile kansa ya utumbo, mifupa na kifo cha ghafla.

Aidha, amesema wataanza kufanya operesheni maalumu kwenye migahawa ili kutoa elimu na kuwakamata wote wanaofanya upishi wa namna hiyo.

 

Serikali yafanya mapitio ya mwongozo wa kilimo cha umwagiliaji
Kamishna Andengenye atoa somo kuhusu mitungi ya Gesi