Serikali ipo kwenye mazungumzo na taasisi ya Tanzania Horticultural Association (TAHA), ili kuangalia namna ya kuuza zao lake la parachichi moja kwa moja bila kupitia nchini Kenya.

Hayo yamebainishwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga kupitia mazungumzo yake aliyoyafanya na na vyombo vya Habari hii leo Septemba 21, 2022 kwa njia ya mtandao wa Zoom.

Amesema, Tanzania huuza parachichi nchi za ulaya ikiwa nyumba ya Afrika ya Kusini na Kenya, lakini sehemu kubwa ya zao hilo hupitia nchi ya Kenya, na kwamba uuzaji wa moja kwa moja utasaidia kukuza pato la mkulima na Taifa kiujumla.

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga.

Aidha, Balozi Nyamanga ameongeza kuwa mbali na zao hilo la Parachichi, pia Tanzania huuza minofu ya samaki nchini Ubeligiji, kwa kusafirisha tani 50 mpaka 60 ambayo husambazwa maeneo mbalimbali ya nchi zingine za bara la Ulaya.

“Tanzania tunauza sana minofu ya samaki nchini Ubeligiji, kwa sasa kupitia minofu ya samaki kutoka Mwanza inaingiza tani 50 mpaka 60 kila wiki ambako inaenda Ubeligiji na kusambazwa nchi zingine,” amesema Balozi Nyamanga.

Ameongeza kuwa, “Ubeligiji mpaka sasa inashirikiana na nchi 14 pekee Duniani kwenye masuala mbalimbali hasa ubia wa maendeleo ikiwemo Tanzania na imekuwa ikitoa karibia Euro milioni 11 kila mwaka kwa Serikalini au NGO’s zao, kwa miradi ya kilimo na maji.

Katika hatua nyingine, Balozi Nyamanga amesema tayari wameongea na wawekezaji kutoka Ubeligiji ambao wanatarajia kujenga kiwanda cha kimea Mkoani Dodoma kwa thamani ya dola zaidi ya milioni 150 na ukamilikaji wake utasaidia kutoa ajira kwa Watanzania.

Amefafanua kuwa, “Ubeligiji ilikuwa na miradi 32 ya uwekezaji mwanzo yenye thamani ya shillingi milioni 902 lakini sasa ina miradi 45 nchini Tanzania yenye thamani ya shillingi milioni 978 ambayo ipo katika maeneo mbalimbali.

Habari kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 22, 2022
Ujenzi bwawa la umwagiliaji kusaidia ukuzaji sekta ya Kilimo