Beki kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Pascal Wawa, amefichua namna majeraha ya goti yalivyomtesa kisaikolojia baada ya kupata hofu kubwa ya kutocheza soka kwa muda wa mwaka mmoja.

Wawa aliyeanza kufanya mazoezi mepesi ya gym jana Jumatano asubuhi chini ya uangalizi wa Mtaalamu wa Viungo wa Azam FC, Sergio Perez Soto, alipata majeraha hayo Aprili 10, mwaka huu wakati timu hiyo ikiichapa Esperance ya Tunisia mabao 2-1 kwenye mchezo wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akifanya mahojiano maalumu na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz, Wawa alisema kuwa akili yake iliathirika baada ya mambo mengi kumjia kichwani kwake juu ya hatima ya soka lake baada ya kupata majeraha hayo.

“Nilipopata majeraha haya nilikuwa nafikiria ndio basi sitaweza kucheza soka, nilikuwa nafikiria natakiwa kufanyiwa upasuaji na nilikuwa na hofu kubwa ya kukaa mwaka mmoja nje ya dimba bila kucheza,” alisema.

“Lakini pia mara baada ya kupata majeraha haya, niliweza kupumzika kwa muda wa takribani miezi miwili kabla ya kwenda Afrika Kusini (Hospitali ya Vincent Pallotti), nilipoenda huko daktari aliuchunguza mguu wangu na kuniambia kuwa nina ‘ligament’ tano katika goti langu, ambapo moja imekatika.

“Aliniambia tatizo langu halihitaji upasuaji, na angefanya hivyo kama ‘ligament’ mbili zingekuwa zimekatika, namshukuru sana Mungu kwani jamno la kwanza nililofanya wiki moja kabla ya kwenda huko niliweza kumwomba Mungu nisikutane na upasuaji,” alisema.

Alichoambiwa na daktari

Nyota huyo wa zamani wa Asec Mimosa na El Merreikh ya Sudan, alisema kuwa mara baada ya uchunguzi huo daktari alimuambia hahitaji matibabu yoyote bali apumzike kwa muda wa miezi miwili.

‘Daktari aliniambia nilale na kula tu kwa muda wa miezi miwili, nilipomaliza uchunguzi Afrika Kusini, nilirejea Dar es Salaam na kuongea na Bosi Yusuf (Bakhresa) na kumweleza nilichoambiwa na daktari, baada ya hapo nilienda kupumzika nchini kwetu kwa mwezi mmoja na nusu na sasa nimerejea tena,” alisema.

Atarejea lini dimbani?

“Nadhani baada ya kumalizika mwezi huu nitaanza kucheza mechi, lakini baada ya wiki moja nitaanza mazoezi uwanjani, hivi sasa mguu wangu uko vizuri ninapokimbia kwa kasi nasikia kawaida, kabla ya hapo nilikuwa napata tabu sana nilipokuwa nikikimbia kwa kasi, nasikia furaha sana hivi sasa hata ukiangalia sura yangu inaonyesha hivyo,” alisema.

Awatuliza mashabiki Azam FC

Baada ya kuanza rasmi mazoezi mepesi ya gym, Wawa amewatuliza mashabiki wa Azam FC kwa kuwaambia kuwa muda si mrefu atarejea na kuwaahidi kuwa atawapa mambo mazuri mengi katika mechi.

“Mashabiki walikuwa na wasiwasi kuwa sitarudi baada ya kutoniona kwa muda mrefu, wasiwe na wasiwasi kwani nimerejea hivi sasa, nitawapa mambo mazuri kwenye mechi, najua nimewapa mambo mazuri mpaka sasa kwa kipindi chote nilichokuwa Azam hadi wakaamua kunipenda, lakini sio sana kulinganisha na mazuri niliyokuwa naonyesha Sudan (El Merreikh).

“Nataka kuonyesha makubwa zaidi hapa, nataka watu wanipende zaidi na kunifikiria kila siku hata kama sitakuwa hapa pale nitakapoenda timu nyingine, lakini nataka watu hapa wamkumbuke Pascal Wawa kama nilivyofanya Sudan,” alisema.

Alisema hata staili mpya ya nywele aliyonyoa, alikuwa akiitumia Sudan na kumpa mafanikio mengi hadi kugeuka kipenzi cha watu wa huko, hivyo anadhani kupitia staili hiyo ataweza kufanya mazuri zaidi msimu ujao.

Amwaga shukrani

Wawa hakuacha kutoa shukrani zake kwa watu waliokuwa naye bega kwa bega kwa kipindi chote alichokuwa akiuguza majeraha, ambapo alimshukuru kwa kiasi kikubwa Mmoja wa Wakurugenzi wa Azam FC, Yusuf Bakhresa, kwa kumpa msaada mkubwa kwenye kipindi hicho.

“Kwanza napenda kumshukuru Mungu, pili napenda kumshukuru mke wangu kwa sababu alikuwa akinisaidia sana na kunipa ushauri, pia namshukuru kwa kiasi kikubwa bosi Yusuf, kwa sababu baada ya kupata majeraha haya alinisaidia sana mimi, alikuwa akinipigia simu kila siku, namshukuru sana kwa kweli,” alisema Wawa aliyejiunga na Azam FC Desemba mwaka juzi akitokea kwa vigogo wa soka Sudan, El Merreikh.

Video Mpya: Dully Sykes Feat. Harmonize
Moussa Sissoko Aendelea Kuiota Real Madrid