Mahasimu wa jiji la Manchester, Man Utd pamoja na Man City wapo katika harakati za kumuwania beki kutoka nchini Serbia, Nikola Maksimovic ambaye yu njiani kuchana na klabu yake ya Torino inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Italia (Sirie A).

Vita ya wawili hao, imeanza kutazamwa kwa uangalifu mkubwa na wadadisi wa soka barani Ulaya, kutokana na klabu zote mbili kuhitaji beki atakayeweza kukidhi haja ya kujenga ukuta mgumu dhidi ya timu pinzani.

Mtandao wa Tuttosport umeandika kwamba, meneja mtarajiwa wa klabu ya Man city, Pep Guardiola anapewa nafasi kubwa ya kumnasa Maksimovic kutokana na mipango ambayo ameanza kuisuka katika kipindi hiki ambacho anamalizia mkataba wake na FC Bayern Munich.

Hatua hiyo ya Guardiola inachukuliwa kama pigo kubwa kwa Man Utd ambao wamejipanga kusubiri mwishoni mwa msimu huu, ambapo watafanya maamuzi ya kuendelea na meneja Louis Van Gaal ama kumuajiri meneja mpya, na ndipo waanze taratibu za usajili wa wachezaji.

Hata hivyo meneja kutoka nchini Ureno, Jose Mourinho ambaye anatajwa huenda akapewa ajira huko Old Trafford mwishoni mwa msimu huu, ni shabiki mkubwa wa beki huyo mwenye umri wa miaka 24.

Wakati purukushani hizo zikiendelea, rais wa klabu ya Torino, Urbano Cairo amesema watakua tayari kusikiliza ofa ya klabu yoyote itakayokua na mvuto, huku akisisitiza thamani ya Maksimovic kuwa ni Euro million 25.

Maksimovic alijiunga na Torino mwaka 2013, akitokea nchini kwao Serbia alipokua akiitumikia klabu ya Red Star Belgrade kwa ada ya uhamisho wa Euro million 4.

Mpaka sasa Maksimovic, ameshaitumikia klabu ya Torino katika michezo sitini na tano (65) na hajawahi kufunga bao.

Antonio Conte Adhamiria Kuvunja Ukuta Wa Real Madrid
Cantona Apindisha Kauli Kuhusu Ajira Yake Olympique Marseille