Meneja mpya wa Man City, Pep Guardiola amekanusha uvumi unaomuandama kwa sasa kuhusu harakati za usajili wa mshambuliaji kutoka nchini Argentina na klabu ya Barcelona ya Hispania, Lionel Messi.

Gurdiola amekanusha taarifa hizo kutokana na baadhi ya vyombo vya habari kuripoti kwamba, yupo katika mpango wa kumuhamishia mshambuliaji huyo Etihad Stadium, kwa ada ya uhamisho ambayo itaweka rekodi duniani.

Meneja huyo kutoka nchini Hispania amesema taarifa hizo sio za kweli na ameshangazwa na zinavyoendelea kuripotiwa kila kukicha.

Amesema hana mpango wa kumsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29, kutokana na kufahamu ugumu wa kuipata saini yake, hasa katika kipindi hiki ambacho ushindani wa soka unaendelea kukua duniani kote.

Guardiola ameongeza kuwa, huenda baadhi ya waandishi wa taarifa za usajili wa Lionel Messi kwenda Man City, wanachukulia ukaribu uliopo kati yao ndio unaweza kufanikisha jambo hilo kwa urahisi.

“Haiwezi kuwa rahisi kwa kiasi hicho, ni vugumu sana kumsajili Messi kutoka FC Barcelona na kumpeleka popote pale ambapo mashabiki wanafikiria.

“Kweli ninakiri nina ukaribu sana na Messi, lakini si kwa kiasi cha kumshawishi aweze kuondoka FC Barcelona, na hata kama itatokea nimefanikiwa kumshawishi, bado kizingiti kitakua kwa viongozi wake.”

Pep Guardiola amepewa jukumu la kukisuka upya kikosi cha Man City tangu alipoanza kufanya kazi yake rasmi klabuni hapo, na tayari ameshawasajili wachezaji wawili.

Waliosajiliwa na meneja huyo aliyekua akiitumikia FC Bayern Munich kabla ya kutimkia Etihad Stadium, ni kiungo kutoka nchini Ujerumani, İlkay Gündoğan  pamoja na mshambuliaji wa Hispania, Manuel Agudo Durán Nolito.

Watzke: Tulistahili Kumuachia Mkhitaryan Aende Old Trafford
5 Kubwa kutoka Magazeti ya Leo