Meneja wa klabu ya Man City Pep Guardiola, amesema kiungo kutoka nchini Ivory Coast Yaya Toure hatocheza tena kwenye kikosi chake, endapo atashindwa kuomba radhi.

Guardiola anataka mchezaji huyo aombe radhi kupitia kwa wakala wake Dimitri Seluk kufuatia maneno makali aliyoyazungumza majuma mawili yaliyopita kutokana na hatua ya jina la kiungo huyo kuenguliwa katika usajili wa wachezaji wa Man City wanaoshiriki ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Wakala wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33, alizungumza na baadhi ya vyombo vya habari na kueleza kwamba, hatua ya kuachwa jina la mchezaji wake ni sawa na kitendo cha udhalilishaji ambacho kimefanywa na Guardiola.

“Napaswa kuombwa radhi, na kama atashindwa kufanya hivyo Toure hatocheza tena katika kikosi changu,” Amesema Guardiola.

“Ilikua vigumu kwangu kuliacha jina la Toure katika usajili wa ligi ya mabingwa, lakini ilinilazimu kufanya hivyo kutokana na idadi ya wachezaji inayotakiwa,

“Nafahamu uwezo wa Toure ni mkubwa kwa sababu nimefanyanae kazi tangu tukiwa FC Barcelona, hivyo halikua kusudio langu kufanya maamuzi ya kumuacha kwa makusudi.” Alisisitiza Guardiola

Guardiola alitoa agizo la kutaka aombwe radhi, dakika chache baada ya Yaya Toure kutangaza kustaafu soka la kimataifa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Toure amechukua maamuzi ya kustaafu kuitumikia timu ya taifa lake la Ivory Coast baada ya kuitumikia tangu mwaka 2004, ambapo amecheza michezo 113 ambayo inajumuisha ile ya fainali za Afrika pamoja na kombe la dunia.

“Nimeandika hivi kwa uchungu, kwa sababu maamuzi haya ni magumu kwangu japo naamini inatosha kuitumikia timu ya taifa langu.” amendika Toure.

Kilimanjaro Queens Yawafuta Machozi Zanzibar Queens
Balaa la mabilioni ya Escrow lamuibua tena Kafulila