Beki wa kati kutoka nchini Ujerumani Per Mertesacker, kwa mara ya kwanza amemzungumzia kiungo aliyejiunga na klabu ya Arsenal, Granit Xhaka kwa kusema mchezaji huyo ni chaguo sahihi la meneja Arsene Wenger.

Mertesacker, ambaye ameshaitumikia Arsenal kwa miaka mitano tangu aliposajiliwa mwaka 2011 akitokea nchini Ujerumani alipokua akiichezea klabu ya Werder Bremen, amesema Xhaka ni mchezaji mwenye kiwango kizuri ambacho kitaweza kuisadia The Gunners kufikia lengo la kufanya vyema msimu wa 2016-17.

Hata hivyo Mertesacker, amekiri kutomfahamu vyema kiungo huyo kutoka nchini Uswiz, kutokana na kutokua mfuatiliaji mzuri wa michezo aliyocheza akiwa katika ligi ya nchini Ujerumani.

“Simfahamu, lakini hilo kwangu sio tatizo kwa sababu nimekua nae hapa katika mazoezi ya kujiandaa na msimu na nimeona kuna kitu cha tofauti anacho ambacho kitatusaidia tutakapoanza msimu mpya wa ligi,” Mertesacker aliiambia Arsenal Player.

Xhaka, alikuwa sehemu ya kikosi cha Uswis ambacho kilishiriki fainali za Euro 2016 zilizofanyika nchini Ufaransa na kuishia katika hatua ya 16 bora.

Xhaka mwenye umri wa miaka 23, alisajiliwa na Arsene Wenger mwezi Mei mwaka huu, akitokea nchini Ujerumani katika klabu ya Borussia Monchengladbach kwa ada ya uhamisho ya Pauni milioni 30.

Alikiba na Diamond Wajifunze Kupitia Maneno ya Jokate Mwegelo
Diego Costa Akanusha Kuondoka Chelsea