Mabingwa wa soka Tanzania Simba SC wamemtambulisha rasmi beki kutoka nchini Zimbabwe Peter Muduhwa akitokea Klabu ya Higlanders FC ya nchini kwao.

Muduhwa ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Zimbabwe kilichoshiriki michuano ya Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’, inayoendelea nchini Cameroon, ametambulishwa rasmi leo mchana, kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za klabu ya Simba.

Mapema hii leo kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za Simba SC, zilitoa taarifa za ujio na utambulisho wa beki huyo, ambaye aliwasili nchini akitokea moja kwa moja Cameron baada ya Zimbabwe kuondoshwa kwenye fainali za ‘CHAN’.

Ikiwa nchini Cameroon, timu ya Taifa ya Zimbabwe imecheza jumla ya michezo mitatu na haijaambulia ushindi kwenye michezo yote ya kundi A.

Imemaliza ikiwa inaburuza mkia wa kundi A, huku ikifungwa jumla ya mabao matano, na safu yake ya ushambuliaji imefunga bao moja pekee.

Kinara wa Kundi A ni Mali mwenye alama 7, wakifuatiwa na mwenyeji Cameroon mwenye alama tano, na ndizo timu mbili pekee zilizofuzu kwa hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kutoka kundi hilo.

PICHA: Al Hilal yatua Dar es salaam
FC Platinum, Bulawayo Chiefs zamchelewesha Chikwende