Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Philip Mangula amezitolea majibu hoja zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa chama hicho kimekuwa kikihofia kumkabidhi kijiti cha uenyekiti wa chama, Rais John Magufuli.

Mangula amepinga hoja hizo na kueleza kuwa hakuna hofu yoyote ndani ya chama hicho kwani ndicho kilichompitisha kugombea urais kikifahamu kiutaratibu ndiye atakayekuwa Mwenyekiti wa chama.

“Kwanza yeye ni rais aliyetokana na uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi. Na chama ndicho kimemuwezesha kupata nafasi ile,” alisema Mangula.

Akizungumzia kile kinachoonekana kama ni ucheleweshwaji wa zoezi hilo la kumkabidhi madaraka ya chama, alisema kuwa kuna utaratibu wa kawaida unaotumika ambao ulitumika pia kwa watangulizi wake wakikaa madarakani zaidi ya miezi sita kabla ya kupewa uenyekiti.

Alisema kuwa Kamati Kuu ya Chama inakutana mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kuunda Kamati mbalimbali zitakazoratibu zoezi la makabidhiano ya Uenyekiti wa chama hicho kwa Rais John Magufuli.

Taarifa zilizotolewa jana na Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka imeeleza kuwa Kamati Kuu ya CCM inaanza kukutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza mchakato wa kumkabidhi Rais Magufuli Uenyekiti wa chama.

Hanscana: Hata kama msanii awe mbaya vipi, asipoonekana mzuri kwenye video hakuelewi
Jukwaa la Katiba lavuta usikivu wa Rais Magufuli