Hatimaye shindano la kumtafuta mrimbwende atakayevaa taji la Miss Tanzania 2019 limekamilika baada ya jopo la majaji kumchagua Sylvia Sebastian kuwa mshindi, katika tukio lililofanyika usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam.

Sylvia ni mhitimu wa kidato cha sita na kwa sasa anasoma kozi ya kompyuta katika Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Mrembo huyo kutoka Mwanza amefanikiwa kupenya katika vipengele vyote ikiwa ni pamoja na uwezo wa kujieleza, ufahamu wa masuala mbalimbali pamoja na jinsi alivyoweza kuutumia uzuri wake wa Kiafrika akiwa jukwaani ndani ya mavazi ya aina tofauti.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo na kushuhudia Sylvia akivishwa taji linalompa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya urimbwende ya dunia (Miss World 2019) yatakayofanyika Desemba 14, London, Uingereza.

Waandaaji wa shindano hilo, kampuni ya The Look wametoa Sh. 10 Milioni kama zawadi kwa Miss Tanzania 2019.

Sylvia amepokea taji hilo kutoka kwa Queen Elizabeth Makune aliyekuwa mshindi mwaka 2018.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 24, 2019
Moto waendelea kuteketeza msitu mkubwa wa Amazon