Wakili wa mchekeshaji maarufu nchini, Idriss Sultan, amesema kuwa msanii huyo anahojiwa na polisi juu ya kuicheka picha ya Rais John Pombe Magufuli.

Kwamujibu wa BBC, Benedict Ishabakaki amesema Sultan hajafunguliwa mashtaka rasmi na polisi na maswali anayohojiwa kufikia sasa yanahusiana na mkanda wa video aliotuma mitandaoni hivi karibuni akionekana akiicheka picha ya zamani ya rais Magufuli.

Ameongeza kuwa anashikiliwa na polisi toka Jumanne mchana punde tu alipoitikia wito wa kuripoti kituo cha polisi na mpaka sasa bado hajapatiwa dhamana wala kupandishwa kizimbani.

“Tunataraji anaweza kuachiwa kwa dhamana hii leo…masharti tuliyopewa ni awe na wadhamini wawili wanaotambuliwa na serikali ya mtaa,” amesema wakili Ishabakaki.

Hii ni mara ya pili kwa mchekeshaji huyo kuingia matatani kwa kutumia picha ya rais Magufuli katika sanaa yake.

Mwezi Oktoba mwaka jana, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alimuamuru kuripoti polisi baada ya kubadili picha yake na ya magufuli.

Michezo kurudi Juni Mosi
Matumaini ya Corona kuisha duniani yaanza kufifia