Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Pierre Lechantre, amesema analijua vilivyo soka la Misri, hivyo amewaomba mashabiki wa soka wa jijini Dar es salaam na sehemu za pembezoni mwa jiji hilo kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kesho wa kombe la shirikisho ambao utawakutanisha na Al Masry katika uwanja wa taifa.

Lenchantre ameeleza suala hilo kwa kujiamini alipokua katika mkutano na waandishi wa habari mapema hii leo jijini humo, ambapo ameongeza kuwa jambo kubwa alilolibaini kwa wapinznai wao kutoka nchini Misri ni ujasiri wa kupambana wakati wote, huku wakiweka lengo la kutangulia kupata bao la kuongoza.

Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amesema ujasiri wa kikosi cha wapinznai wake pia umekua chagizo katika ushindani kwenye ligi yao nchini kwao Misri, jambo ambalo limewasababishia kuwa na kikosi kizuri cha timu ya taifa ambacho kimefuzu kucheza fainali za kombe la dunia.

Hata hivyo kocha huyo mwenye umri wa miaka 67 amekimwagia sifa kikosi chake kwa kusema kipo vizuri na kimeonyesha utayari wa mpambano wa kesho wa michuano ya kombe la shirikisho, lakini akagusia suala la uzoefu ambalo huenda likawa changamoto kwa wachezaji wake kutokana na kukosa nafasi ya kushiriki kimataifa kwa muda mrefu.

Mbali na hilo, Lechantre amesema pia ni vyema wakatumia faida ya uwanja wa nyumbani kushinda ili wakienda kucheza mchezo wa marudiano iwe rahisi kusonga mbele.

Lechantre ameongeza kuwa timu inapotumia uwanja wa nyumbani vizuri, uhakika wa kusonga mbele unakuwepo kutokana na ugumu unaokuwepo mechi za ugenini.

Kwa upande wa nahodha na mshambuliaji kikosi cha Simba John Bocco ameungana na kocha wake kwa kutoa wito kwa mashabiki wa soka kufika uwanjani bila kukosa, ili kuwapa hamasa hiyo kesho na kufanikisha lengo la kuibuka na ushindi kwenye uwanja wa nyumbani.

Bocco amesema kwa ujumla wachezaji wote wa kikosi cha Simba wapo katika mazingira mazuri na wana ari ya kupambana na Al Masry hiyo kesho, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanawafurahisha mashabiki wa soka nchini kwa kupigana hadi tone la mwisho.

Wakati huo huo mkuu wa idara ya habari na mawasilino wa klabu ya Simba Haji Sunday Manara amesema kwa ujumla maandalizi ya mchezo wa kesho dhidi ya Al Masry yameshakamilika na kinachosubiriwa ni waamuzi kutoka Afrika Kusini kupuliza kipyenga ndani ya dakika 90.

John Bocco: Historia inatubeba kwa waarabu
Waziri wa elimu ahusishwa na ufisadi