Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo Septemba 5, 2018 amekutana na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Pius Msekwa na Mkewe Mama Anna Abdallah ambaye ni Waziri Mstaafu katika Ikulu Ndogo ya Nansio Ukerewe mkoani Mwanza.

Baada ya mazungumzo yao Mzee Msekwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kufanya ziara yake ya kwanza katika kisiwa cha Ukerewe tangu achaguliwe kuwa Rais, na kwa Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kisiwani humo ikiwemo Maji, ujenzi wa barabara na ununuzi wa meli mpya katika ziwa Victoria.

Mhe. Msekwa pia amezungumzia utendaji kazi wa Mhe. Rais Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano, ambapo amesema mageuzi makubwa yanayofanywa yanaandika historia kama alivyofanya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

“Kwa Nyerere tulisema kama sio juhudi zako Nyerere, maendeleo tungepata wapi, na huyu Rais Magufuli naye tutasema kama sio juhudi zako meli, Dreamliner, reli na mengine mengi tungepata wapi?” amesisitiza Mzee Msekwa.

Kwa upande wake Mama Anna Abdallah amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa ya kujenga uchumi na kuwapa nafasi za uongozi wanawake wengi, na ametoa wito kwa wanawake wote waliopata nafasi za uongozi kuonesha mfano mzuri kwa kuchapa kazi kwa juhudi, uadilifu mkubwa na kujiamini ili wengine wengi zaidi waendelee kupata nafasi.

“Nafurahishwa sana na kazi zinazofanywa na Mhe. Rais Magufuli, kwa hakika anatutendea mazuri mengi sana sisi Watanzania na sisi wanawake” amesema Mama Anna Abdallah.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa.

JPM aagiza kutumbuliwa kwa Kamishna wa Ardhi Kanda ya Ziwa
Ommy Dimpoz aombewa dua, ushirikina upo.