Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amemjibu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe aliyedai chama hicho kwa kushirikiana na Serikali wamehujumu chaguzi ndogo.

Polepole amesema kuwa CCM hivi sasa imejikita katika kutekeleza ahadi zake kwa wananchi na kwamba hawana muda wa siasa za ‘maji-taka’.

Alitamkata Mbowe kutomtafuta mchawi nje ya chama chake na kudai kuwa anayehujumu demokrasia ya nchi ni anayetaka kuleta taharuki huku familia yake ikiwa salama.

“Mbowe asitafute mchawi nje ya chama chake na yeye mwenyewe. Anayetuharibia wito wa demokrasia sasa hivi ni mtu ambaye anazungumzia kubeba majeneza ya Watanzania, mbona hajazungumza kubeba majeneza ya watoto wake?” Alihoji.

“Anapiga mawe polisi na kuwandamanisha watu wakati watoto wake wako salama,” Polepole aliongeza.

Aidha, alisema kuhusu suala la Sugu, matamshi ya Mbowe yanaonesha kuwa ni mtu mnafiki kwani Mahakama inapotoa maamuzi yanayompa ahueni mbunge wake anaisifia lakini inapotoa hukumu inayomfunga mbunge wake kwa kutoa maneno ya uchochezi anaishambulia.

Awali, Mbowe alidai kuwa Polisi na Serikali wana mpango wa kuwapa kesi ya maandamano inayohusiana na kifo cha mwanafunzi wa NIT, Akwilina Akwiline.

Kiongozi huyo wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni alipinga uamuzi wa Mahakama kumfunga Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi kifungo cha miezi mitano jela akidai ilitokana na shinikizo kutoka juu.

Waziri Mkuu achunguzwa kesi ya uhujumu uchumi
Polisi ahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kuwapiga risasi waandamanaji

Comments

comments