Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Humphrey Polepole amewataka vijana wa chama hicho kuendelea kuwa na ujasiri, umoja na mshikamano katika kulinda na kutetea maslahi ya Chama na Taifa pamoja na kuepuka vikao visivyo na maana.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Vijana wa CCM mkoani Mwanza katika uzinduzi wa kampeni ya “Nyamagana ya Kijani”

”Nasisitiza viongozi wanaokiuka misingi ya maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama hakitasita kuwachukulia hatua viongozi wenyewe au vikao ambavyo vitakwenda kinyume na misingi ya CCM,”amesema Polepole.

Aidha, Polepole ametolea mfano vikao hivyo kuwa ni kama vile vitakavyoweka msimamo wa kumbeba mwanachama mgombea na kwamba vikao hivyo vitachukuliwa hatua pia ili kulinda nidhamu ya chama.

Pia, Polepole amewaeleza vijana wa CCM kuwa wao ni ngao ya viongozi wa CCM, hivyo waendelee kumlinda, kumtetea na Kumuunga Mkono Rais, John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wa chama hicho na kuwapinga viongozi wanaotaka kumuangusha kwa hila na wasiofuata utaratibu kupitia vikao.

Mwigulu Style inatosha kuwa vazi la taifa- Dkt. Nchemba
Mahari kubwa yatajwa kuwa kikwazo cha vijana kuoa