Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amelaani vikali kauli iliyotolewa na mtangulizi wake ambaye ni mbunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye kuwa alisaidia kukitoa chama hicho shimoni.

Nape alitoa kauli hiyo dakika chache baada ya mkutano wake na waandishi wa habari kuzuiwa na kutishiwa bastola na mtu mmoja, siku moja baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya Uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Polepole alisema kuwa kauli hiyo ya Nape sio kauli sahihi ya kiongozi na kwamba yeye pekee hawezi kukitoa chama shimoni huku kukiwa na wanachama milioni nane na maelfu ya viongozi.

Mwanachama anayejitambua hawezi kusema anakibeba chama, wanachama wote milioni nane walikuwa wapi? Viongozi wote maelfu walikuwa wapi? Nape ni kiongozi wetu kwenye chama, kama kweli alisema maneno hayo alikengeuka sana,” Polepole anakaririwa na Mwananchi.

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM alisema kuwa Kamati ya Maadili inapaswa kuliangalia suala hili na kumchukulia hatua Nape.

“Tuna kila sababu za kumshauri Mzee Mangula wa Kamati ya maadili kuwa hatuwezi kuwa na viongozi wa aina hii. Chama chenye watu milioni nane unakitoa shimoni na nini? Unakitoa na ngazi, ulitumia kamba kukitupia shimoni, uliita zimamoto? Alihoji.

Hata hivyo, Polepole alisema kuwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa viongozi kama Nape sio za kuwawekea ukomo bali kuwalea kimaadili kwa kutumia hekima na busara ili watambue kuwa chama sio punda anayeweza kutumbukia shimoni. Hivyo, alisema CCM iko kwenye mpango wa kuanzisha chuo kikuu kitakachotoa mafunzo kwa makada wake kuhusu nidhamu na maadili.

Video: CCM 'wamshtaki' Nape, CUF walia na jeshi la Polisi
Magazeti ya Tanzania leo April 25, 2017

Comments

comments